Talaka sababu ya ulawiti kwa watoto Pangani
10 June 2024, 9:51 pm
Matukio ya ukatili ikiwemo ulawiti, inatajwa kuendelea kutokea ingawa jitihada za wadau zikifanyika dhidi ya matukio hayo huku utelekezaji familia, ushirikina na wazazi kutengana zikitajwa kuwa ni sababu.
Na Cosmas Clement
Shirika la Uzima kwa Sanaa (UZIKWASA) lililopo wilayani Pangani mkoani Tanga limewakutanisha wajumbe wa kikosi kazi wilayani humo ili kujadili, kutathmini na kuibua mikakati ya kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Wakizungumza katika kikao hicho wajumbe hao wameelezea kuguswa na matukio ya ukatili, ubakaji na ulawiti yanayotokea wilayani humo yanayopelekea kuharibu ndoto na maisha ya watoto.
Miongoni mwa sababu zilizotajwa na wajumbe hao ni pamoja na wazazi kutengana, utelekezaji wa watoto, imani za kishirikina pamoja na tabia ya baadhi ya wazazi kulala pamoja na watoto wao.
Kwa upande wake mwezeshaji kutoka shirika la UZIKWASA bwana Nickson Lutenda amewasihi wajumbe hao kuangalia namna bora ya kushughulikia matukio hayo bila ya kuathiriwa na dhana binafsi.
Mwezeshaji mwingine kutoka UZIKWASA Bi Salvata Kalanga amewataka wajumbe hao kutengeneza mkakati wa pamoja kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia.
Kikao hicho ni muendelezo wa shughuli za shirika la UZIKWASA katika kuwawezesha wadau mbalimbali kuboresha utendaji katika kukabilina na vitendo vya ukatili, ambapo miongoni mwa wanaounda kikosi kazi hicho ni wawakilishi kutoka idara mbalimbali za halmashauri, Mkuu wa Wilaya na jeshi la polisi.