Pangani FM
Pangani FM
08/03/2026, 19:27

Na Cosmas Clement/Catherine Sekibaha
Shirika la Earth Lungs Restoration Foundation hii leo limeadhimisha siku ya wanawake duniani kwa kukutana na kuwapongeza wanawake wanaojihusisha na upandaji wa mikoko kutoka maeneo ya Pangani magharibi na Mkwajuni/Msaraza wilayani Pangani.
Katika kuadhimisha siku hiyo shirika hilo limetembelea maeneo yanayopandwa mikoko na wanawake hao wilaya ya Pangani ambao wanaendesha shughuli za upandaji wa mikoko kwa mkataba na Earth Lungs Restoration Foundation.
Akizungumza na Pangani fm afisa matokeo ya jamii kutoka shirika la Earth Lungs Restoration Foundation Bi Huruma David amesema wanawashirikisha wanawake katika utunzaji wamikoko kwa kuwa ni watu wenye uwezo wa kuleta mabadiliko katika jamii dhidi ya mabadiiko ya tabia nchi .
Kwa upande wao wanawake ambao ni wanufaika walioshiriki katika maadhimisho hayo, wamelishukuru shirika la Earth Lungs Restoration Foundation kuwajumuisha katika mradi huo kwani imewasaidia katika kuwapatia kipato na kuimarisha mazingira ya fukwe na maeneo ya mikoko katika maeneo yao.
Naye Afisa misitu kutoka kata ya Bushiri wilayani Pangani Bi Adelade Swai amelipongeza shirika hilo akisema limekuwa na mchango mkubwa katika kuwahusisha wanawake katika utunzaji wa mazingira na kuwezesha kuleta matokeo chanya katika kutunza misitu ya mikoko wilayani Pangani.
Shirika la Earth Lungs Restoration Foundation ni shirika lisilo la serikali ambalo kwa nchi ya Tanzania linaendesha shughuli zake katika wilaya za Pangani, Mkinga, Tanga pamoja na Bagamoyo mkoani Pwani.