Pangani FM
Pangani FM
16 July 2025, 10:45 am

“Kuna watu wanasema miti na binadamu inategemeana sasa tukiikata hii miti tutaishije?”
Na Catherine Sekibaha
Wananchi wilayani Pangani mkoani Tanga wametakiwa kutunza mazingira ili kunusuru hali ya uharibifu iliyopo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Wakizungumza wakati wa mafunzo ya Mguso yaliyotolewa na shirika la UZIKWASA kwa kamati ya mazingira kijiji cha Mtonga, baadhi ya wajumbe hao wamekiri kuchangia uharibifu huo na kujipanga upya kushirikiana kutunza mazingira yao.
Kwa upande wake Mwezeshaji kutoka shirika la UZIKWASA Bi. Salvata Kalanga amewataka wanakamati hao kuwa mfano mzuri katika kuacha shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira ili vizazi vijavyo viweze kunufaika na uwepo wa ardhi nzuri.
Bi. Agnes Abel Makaranga ni Afisa Tabibu wa zahanati ya Mtonga, amewaasa wananchi wa eneo lake kuhakikisha wanatunza mazingira yao pamoja na kupanda miti ili kupata hewa safi.
Mafunzo ya Uongozi wa Mguso yametolewa kwa kamati za mazingira ili kumuwezesha kiongozi mmojammoja kuguswa na uharibifu uliofanyika katika eneo lake na kubuni mbinu thabiti ya kupunguza uharibifu huo ili kurejesha hali ya uoto iliyopotea.