Pangani FM
Pangani FM
12 May 2025, 11:59 am

Miaka mitatu iliyopita kijiji cha Kigurusimba kilichopo wilayani Pangani, kilikuwa ni miongoni mwa vijiji vilivyokuwa hatarini kwa magonjwa ya mlipuko kutokana na kaya nyingi kutokuwa na vyoo bora.
Na Cosmas Clement
Wajumbe wa kamati ya MTAKUWWA ya kijiji cha Kigurusimba wilayani Pangani mkoani Tanga, wamesema wamefanikiwa kupunguza hatari ya magonjwa ya mlipuko kutokana na kuwawezesha wananchi kujenga vyoo bora kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na utekelezaji wa Mpango kazi wao uliandaliwa baada ya mafunzo yaliyotolewa na shirika la UZIKWASA miaka mitatu iliyopita na kuibuliwa changamoto ya wanajamii kujisaidia maeneo ya mto Pangani, kutokana na idadi kubwa ya kaya kukosa vyoo bora.
Wakizungumza wakati wa zoezi la ufuatiliaji na tathmini katika kijiji hicho wajumbe wa kamati hiyo wamesema kwa sasa wanajivunia kupunguza magonjwa ya mlipuko kwakuwa zaidi ya asilimia 80 ya kaya zimejenga vyoo bora tofauti miaka mitatu iliyopita.
Mganga Mfawidhi wa zahanati ya kijiji hicho Dkt. Neema Mzava amekiri kupungua kwa magonjwa hayo ya mlipuko kwa wakazi hao hivyo kuimarisha afya na kupata muda mwingi wa kujitafutia kipato.