Aweso akabidhi zawadi shilingi Mil.2 kwa waandishi wa habari Pangani FM
11 December 2024, 4:50 pm
Mhe. Aweso ametoa Fedha hizo Kwa ajili ya motisha na zawadi kwa waandishi wa habari wa Pangani FM Baada ya kufanya vema katika tuzo za EJAT.
Na Mwandishi wetu
Leo, December 11 2024, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Pangani, Bw. Salmin Mmari, amemwakilisha Mbunge wa Pangani, Mheshimiwa Jumaa Aweso, katika kukabidhi zawadi ya Shilingi Milioni Mbili kwa waandishi wa habari wa Pangani FM waliobeba ushindi kwenye Tuzo za Umahiri wa Habari Tanzania 2024 (EJAT).
Zawadi hiyo imetolewa na Mheshimiwa Mbunge kwa lengo la kuongeza hamasa kwa waandishi wa habari wa Pangani FM ili waendelee kufanya kazi kwa weledi na ubunifu.
Pia, ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za UZIKWASA katika kuimarisha maendeleo ya jamii ya Pangani kupitia vyombo vya habari na kampeni za mabadiliko ya kijamii.
Bw. Mmari ametoa salamu za pongezi kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge kwa Shirika la UZIKWASA kutokana na juhudi endelevu za kuleta maendeleo ya kijamii, kuhimiza usawa wa kijinsia, na kuhakikisha jamii inalindwa dhidi ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto.
Katika nyakati mbalimbali, Mheshimiwa Mbunge ameshiriki moja kwa moja katika shughuli za UZIKWASA na kuendelea kuunga mkono miradi ya shirika hilo, huku akisaidia kutangaza kazi zake kwa ngazi za juu.
Mkurugenzi wa UZIKWASA, Bw. Novartus Urassa, alipokea salamu za pongezi hizo huku akitoa wito wa kuimarisha mashirikiano kati ya Mbunge na shirika hilo.
Amesisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuongeza nguvu za pamoja kwa maendeleo ya Pangani na kuhakikisha jamii inakuwa salama ambako wanawake na watoto wanaweza kufanikisha ndoto zao.
Pia, alionyesha umuhimu wa kushirikiana katika kuhifadhi mazingira na kujenga ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Mnamo Septemba mwaka huu, waandishi wanne wa Pangani FM, kituo kinachosimamiwa na UZIKWASA, walishinda tuzo za umahiri wa uandishi wa habari zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Ushindi huo umeendelea kuimarisha Pangani FM kama moja ya vyombo vya habari vinavyoheshimika nchini, huku ikiitangaza Pangani kitaifa kwa heshima kubwa