Madiwani Pangani DC waaswa kuongeza nguvu ukusanyaji wa mapato
3 August 2024, 4:11 pm
Mwaka wa fedha 2023/24 halmashauri ya wilaya ya Pangani ilikuwa asilimia 95 ya makisio ya bajeti kwa mwaka huo wa fedha.
Na Cosmas Clement
Wataalamu na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani wameaswa kuboresha kiwango cha ukusanyaji wa mapato katika mwaka wa fedha 2024/25.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Pangani ya Pangani Mussa Kilakara kufuatia halmashauri hiyo kushindwa kufikia asilimia mia moja ya makusanyo ya ndani kwa mwaka 2023/24.
Akizungumza katika kikao cha robo ya nne ya mwaka mkuu huyo wa wilaya amewaasa wataalamu na madiwani hao kudhibiti na kulinda vyanzo mbalimbali vya mapato ya halmashauri.
Amewaomba madiwani kutilia mkato upatikana wa mikopo ya asilimia kumi za halmashauri kwa vikundi vilivyo hai na vyenye tija ili kuepuka ukwamishwaji wa kurejesha mikopo hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani Mheshimiwa Akida Bahorera amesema Halmashauri hiyo imeweka mikakati madhubuti ya kushughulikia changamoto zilizosababishwa ukusanyaji wa mapato usifikie 100% katika mwaka huu wa fedha 2023/2024.
Halmashauri ya wilaya ya Pangani kwa mwaka 2023/24 ilipanga kukusanya na kutumia mapato ya ndani ya shilingi bilioni moja nukta tisa.