Wilaya ya Pangani waaswa kutunza mikoko
27 July 2024, 1:19 pm
Misitu ya mikoko ina uwezo mkubwa wa kuchuja hewa ya ukaa kwa wingi ukilinganisha na aina zingine za miti.
Na Cosmas Clement
Shirika la CAN Tanzania kupitia mradi wa uhifadhi na urejeshaji wa misitu kwa njia za asili na shirikishi, pamoja na BMU ya kijiji cha Msaraza, Julai 26, 2024 wameadhimisha siku ya mikoko duniani, kwa kutoa elimu ya uhifadhi wa misitu ya mikoko katika kijiji cha Msaraza wilaya ya Pangani mkoani Tanga.
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya mikoko duniani yaliyofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi ya zamani ya Bushiri wilayani Pangani, mratibu wa mradi huo Bi. Sharon Kishenyi amewaasa wanajamii wanaozungukwa na misitu ya mikoko kuilinda ili iendelee kuleta tija katika mazingira.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili ya kijiji cha Msaraza Bw. Anold Boniface amesema pamoja na kuadhimisha siku kwa kushirikiana na kamati ya BMU ya kijiji hicho, wataendelea kutekeleza afua za kutoa elimu kwa jamii ili kuendeleza misitu ya mikoko.
Naye Afisa Uvuvi kutoka Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi halmashauri wilaya ya Pangani Bi. Erica Cornel ameeleza umuhimu wa uhifadhi na uendelezaji wa mikoko ikiwemo kuwezesha kuzaliana kwa samaki na kuzuia mmonyoko wa fukwe.
Pamoja na shughuli hizo, katika maadhimisho wananchi wamepatiwa majiko banifu ambayo hutumia kuni chache hivyo kupunguza athari za ukataji wa miti kwa ajili ya kuni.
Shirika la CAN Tanzania na UZIKWASA wamekuwa wakishirikiana kwa muda mrefu katika kutekeleza shughuli mbalimbali zinazowezesha kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na utunzaji wa mazingira.