Pangani FM

Wazazi Pangani waaswa kusimamia maadili kwa watoto

22 July 2024, 6:00 pm

Katibu wa mbunge wa jimbo la Pangani Bwana Waziri Mbezi akikabidhi msaada kwa mzee wa kijiji cha Boza.

Mmonyoko wa maadili kwa watoto imekuwa ni ajenda inayozungumzwa kila uchao kutokana na uwepo wa matukio mbalimbali yanayosababaishwa na mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Na Hamisi Makungu

Mbunge wa Jimbo la Pangani Mhe. Jumaa Hamidu Aweso amewataka akina mama kulipa nafasi suala la malezi ya watoto wao, ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili ndani ya jamii.

Ujumbe huo wa Mhe. Aweso umetolewa kwa niaba yake na Katibu wake Bwana Waziri Mbezi alipomuwakilisha kwenye Sherehe za kutimiza Miaka Kumi kwa Kikoba cha EBENEZA GROUP Kijiji cha BOZA.

Katika Salamu zake Mhe. Aweso amewataka kinamama kukaza Kamba katika malezi ya watoto na vijana wao dhidi ya mmomonyoko wa maadili.

Sauti ya bwana Waziri Mbezi katibu wa Mbunge wa jimbo la Pangani

Akizungumza kwenye sherehe hizo Mwenyekiti wa Kijiji cha Boza Geofrey Kalala, amesema mbali na mafanikio mengine ambayo kina mama hao wanayoyapata katika kikoba, amewahimiza umuhimu wa kuwekeza katika elimu kwa watoto wao.

Sauti ya mwenyekiti wa kijiji cha Boza bwana Kalala

Baadhi ya kinamama kutoka Kikundi hicho cha EBENEZA mbali na kuelezea mafanikio yao tangu walipojiunga na Kikoba hicho, pia wamewashauri wanawake wenzao kujiunga katika vikundi ili kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi.

Sauti ya wananchama wa kikundi

Katika kusherehekea kutimiza miaka kumi kikundi cha EBENEZA kilitoa zawadi kwa Bibi mwenye mahitaji maalum, huku wageni na wadau mbalimbali nao wakijitolea kiwango tofauti cha fedha taslim kwa ajili ya kumsaidia Bibi hiyo.

Kikundi hiki cha Kijamii cha Huduma ndogo za kifedha EBENEZA BOZA kilianzishwa June 2014 na kusajiliwa rasmi May 23-2024 kikiwa na dhumuni la kuweka na kukopeshana ili kuwekeza miradi ya kujikwamua kiuchumi na kugawana faida kila Mwaka.