Pangani DC yafikia 77% ya mapato 2023/24
17 May 2024, 5:12 pm
Ukusanyaji wa mapato ndiyo msingi wa huduma bora kwa wananchi, watendaji wa halmashauri ongezeni nguvu katika makusanyo.
Na Cosmas Clement
Halmashauri ya wilaya ya Pangani imesema imefanikiwa kukusanya asilimia 77 ya bajeti ya mapato ya ndani, kupitia mapato lindwa na yasiyolindwa katika mwaka wa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka fedha iliyoishia mwezi machi mwaka 2024.
Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani cha robo tatu ya mwaka wa fedha 2023/2024 kilichofanyika Ijumaa Mei 17 2024, mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Pangani Mhe. Akida Bahorera amesema wanatarajia kufikia malengo ya asilimia mia moja ya makusanyo ifikapo robo ya mwisho wa mwaka huu wa fedha.
Aidha Mhe. Bahorera amewaagiza watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Pangani kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato ili kuweza kutimiza lengo la kufikia asilimia mia moja ya ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Pangani Bwana Mussa Kilakala amewaagiza madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Pangani kushauri vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza mapato na kuboresha huduma kwa jamii.
Wakati wa kuanza mwaka huu wa fedha 2023/2024 halmashauri ya wilaya ya Pangani ilikadiri kukusanya na kutumia fedha za mapato ya ndani kiasi cha shilingi bilioni 1,947,973,000 na mpaka mwezi machi mwaka 2024 makusanyo yakifikia shilingi billion 1,497,851,857 ingawa kwa miezi miwili mpaka mwezi wa tano kiwango cha mapato kinatajwa kupanda.