Serikali yaagiza kuzibwa kwa shimo lililoua Pangani.
15 March 2021, 12:46 pm
Serikali Wilayani Pangani Mkoani Tanga imetoa maelekezo kwa uongozi wa kijiji cha Madanga Wilayani humo kuanza mchakato wa kziba shimo kubwa lililopo kijijini hapo linalofahamika kama ‘shimo la mreno’.
Wenyeji wa kijiji hicho wamedai kuwa shimo hilo limekuwepo tangu kipindi cha ukoloni na bado kina cha shimo hilo hakifahamiki.
Siku ya Jumamosi tarehe 14 mwezi Machi, Jeshi la zimamoto lilifanikiwa kuokoa mwili wa mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina Mmarika Jumaa anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 45 mpaka 50 mkazi wa Kijiji hicho ambaye alitumbukia katika shimo hilo.
Katibu tawala Wilaya ya Pangani Mwalimu Hasani Nyange ni moja ya viongozi waliofika katika eneo la tukio.
Baada ya kufanikiwa kuokoa mwili huo ametoa maelekezo kwa Uongozi wa kijiji hicho kuziba shimo hilo.
‘Sisi kama Serikali ya Wilaya tunawashukuru Jeshi la zimamoto na Wananchi wote lakini tumewapa maelekezo Diwani , Afisa tarafa , mtendaji wa kata na kijiji na mwenyekiti wa Kitongoji wahakikishe badala tu ya kufyeka hili eneo na kuzungushia uzio watafakari namna ya kuliziba kwa juu, lizibwe lote”‘
Amesema Mwalimu Nyange.