Sekondari ya Funguni yajipanga kuongeza Ufaulu 2021
2 March 2021, 3:25 pm
Katika kuhakikisha wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Funguni iliyopo Wilayani Pangani Mkoani Tanga wanafanya vizuri katika matokeo yao ya kidato cha pili na cha nne kwa mwaka 2021, Uongozi wa shule hiyo umekutana na wazazi, walezi pamoja na viongozi wa kata zinazoizunguka shule hiyo ili kujadili masuala mbalimbali ya kimaendeleo kuhusu shule hiyo.
Akizungumza mara baada ya kikao hicho Mkuu wa shule hiyo Mwalimu NASSOR GAMBA mbali na kuwashukuru wazazi kwa kuitikia wito, pia amewataka wazazi kuendelea kushirikiana na walimu katika Jitihada zinazofanywa ili kufikia lengo.
“Tumewafikishia swala zima la taaluma kwa mwaka jana na tunashukuru wazazi na walezi wamelipokea vizuri na kutuunga mkono na wametupa ari katika kuhakikisha tunafanya vizuri huku tukiwaomba kuweza kuchangia michango kwa ajili ya chakula pamoja na watoto kuweza kukaa kambi”
Amesema Mwalimu Gamba.
Kuhusu Miundombinu ya Shule hiyo, Mwl GAMBA amepongeza jitihada za wadau mbalimbali waliochangia, huku akishauri kuendelezwa kwa ushirikiano uliopo hasa katika kukabiliana na changamoto hiyo.
Kikao hicho kati ya Walimu, wazazi, walezi pamoja na Viongozi wa Kata za Pangani Mashariki na Magharibi kimekaliwa Mwishoni mwa Wiki iliyopita.