Viongozi wa Dini watakiwa kuendelea kukemea vitendo vya Ukatili.
1 February 2021, 7:16 pm
Viongozi wa dini wilayani Pangani wametakiwa kuendelea kukemea vitendo vya ukatili katika jamii.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Miaka 100 ya Mahakama Katibu tawala wa wilaya kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ,Mwalimu Hassani Nyange amehimiza juu ya swala la waumini wa Dini mbalimbali kupewa mafundisho yatakayochangia vita dhidi ya vitendo vya Ukatili.
“Kwa mara nyingine tuongee na waumini wetu juu ya vitendo hivi,mfano mnaweza mkakaa na kuona hili jambo kuna uwezekano mtu huyu amefanya,lakini akipelekwa humo ndani (mahakamani) anakataa anasema hamjui huyo mtu,hivi kama mtu mwenyewe kasema hamjui hakimu anamfungaje huyo mtu miaka 30,hivyo tuongee na waumini wetu juu ya halihalisi ya hali kwa sasa ilivyo”
Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Pangani Mheshimiwa William Mnguto amesema kwa sasa wamefanikiwa kumaliza mashauri kwa wakati yanayofikishwa mahakamani kama taratibu zinavyowahitaji.
“Hadi sasa wilaya ya Pangani hatuna kesi iliyozidi mwaka mmoja na mahakama ya mwanzo hakuna kesi iliyozidi miezi 6 kesi zote zimeishia chini ya miezi 3,ambapo mahakama pia imeanzisha kituo cha usuluhishi ambacho kinashughulikia mashauri yaliyo tayari kwa usuluhishi”
Maadhimisho ya kilele cha wiki ya sheria kwa wilaya ya Pangani yamefanyika katika viwanja vya mahakama ya wilaya mjini Pangani ,na kitaifa maazimisho hayo yalifanyika Mkoani Dodoma ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kauli mbiu kwa mwaka huu ilikuwa ni MIAKA 100 YA MAHAKAMA KUU: MCHANGO WA MAHAKAMA KATIKA KUJENGA NCHI INAYOZINGATIA UHURU, HAKI, UDUGU, AMANI NA USTAWI WA WANANCHI 1920 2020 ”.