Sengerema FM

Polisi Mwanza kumsaka aliyeiba mtoto kanisani

30 October 2026, 7:31 pm

Kamanda wa Polisi mkoa Mwanza DCP Wilbroad Mtafungwa.Picha na jeshi la Polisi Mwanza

Kufuatia tukio la kuibiwa mtoto mchanga katika kanisa la Living Water Mwanza, jeshi limetangaza kuanza msako mkali kumtafta aliyehusika na tukio hilo.

Na;Emmanuel Twimanye

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamsaka Mwanamke anayedaiwa kuiba Mtoto wa kiume mwenye umri wa miezi mitatu ndani ya Kanisa la Living Water, lililopo Mtaa wa Kiseke “A”, Kata ya Kiseke, Wilaya ya Ilemela, Jijini Mwanza.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kamanda wa Jeshi la polisi Mkoani Mwanza Wilbroad Mtafungwa,  tukio hilo limetokea majira ya saa 7 mchana , wakati Mama wa Mtoto huyo, Godliver Bahati Zilahenda (23) alipokuwa Kanisani pamoja na mumewe, Galuma Kawekamo.

Inadaiwa kuwa wakati wa kutoa sadaka, Mwanamke huyo alimwomba Mama wa Mtoto amshikie Mtoto wake, ambapo Mama huyo aliporejea kutoka kutoa sadaka, alibaini kuwa Mwanamke huyo ametokomea kusikojulikana na mtoto   .

Baadhi ya wananchi wamesikitishwa na tukio hilo na kuiomba serikali kumsaka na kumkamata mwanamke huyo anayedaiwa kuiba mtoto na kumchukulia hatua kali za kisheria ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hiyo.

Sauti ya Baadhi ya wananchi wilayani Sengerema wakizungumzia wizi wa mtoto.

Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi Mkoani humo linafanya uchunguzi baada ya miili ya Watoto wawili wa kiume, inayokadiriwa kuwa na umri wa miezi mitano hadi sita, kukutwa imetelekezwa kando ya Barabara katika Mtaa wa Chamwenda, Kata ya Nyasaka, Wilaya ya Ilemela.

Aidha miili hiyo ilikutwa   imetelekezwa   majira ya saa 12 jioni, baada ya Polisi kupata taarifa kutoka kwa wananchi.