Sengerema FM

Ajinyonga baada ya kutelekezewa watoto saba na mke wake

6 December 2023, 7:11 pm

Picha ya mtandaoni

Matukio ya wanandoa kuachana yanazidi kushika kasi wilayani Sengerema huku yakitanjwa kuwa ndio chanzo kinacho pelekea vifo kwa baadhi yao baada ya kutalakiana kufuatia msongo wa mawazo na kusindwa kuvumilia maumivu .

Na:Emmanuel Twimanye.

Mwanaume mwenye umri wa miaka 37 katika kijiji cha Tabaruka Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza amefariki Dunia kwa kujinyonga kwenye mti wa mwembe kwa madai ya kushindwa kuwalea watoto saba aliyoachiwa na mke wake baada ya kuachana.

Baadhi ya ndugu wa marehemu na wananchi wamesikitishwa na  maamuzi ya  kujinyonga kwa mwanaume huyo na kuiomba jamii kuacha kuchukua mamauzi ya  kujitoa uhai.     

Mwanamke aliyeachana na marehemu amesema kuwa waliachana baada ya kutokea mgogoro katika ndoa ,huku akikataa  kuwachukua watoto wake kwenda kuwalea kwa madai kuwa wakalelewe na bibi yao licha ya baba yao kufariki Dunia.

Baadhi ya watoto wa marehemu wamesema kuwa baba yao aliwaagiza kwenda kukoboa mpunga   na kwamba waliporudi nyumbani hawakumkuta ndipo walipopata taarifa kutoka kwa majirani zao kuwa baba yao amefariki Dunia kwa kujinyonga .

Mwenyekiti wa kitongoji cha Tabaruka ya Zamani lilipotokea tukio hilo Abdallah Masasila  amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutaja jina la mwanaume aliyefariki kuwa ni   Kiswalucha Sokola mkazi wa kitongoji hicho.

Hata hivyo Jeshi la polisi Wilayani Sengerema limefika eneo la tukio na kuruhusu kufanyika kwa  taratibu za mazishi .