Marufuku kwenda na watoto kwenye kumbi za Starehe
4 April 2024, 4:26 pm
Kutokana na kkuongezeka kwa mmomonyoko wa maadili kwa watoto nchini Serikali ya mtaa wa Migombani Imepiga marufuku wazazi kwenda na watoto kwenye kumbi za Starehe mjini Sengerema
Na:Emmanuel Twimanye
Serikali ya mtaa wa Migombani Kata ya Nyampulukano Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza imepiga marufuku wazazi kwenda na watoto sehemu za starehe ili kuepuka wimbi la mmomonyoko wa maadili kwa watoto.
Marufuku hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa mtaa wa Migombani Anton Busumabu kufuatia kukithiri kwa baadhi ya wazazi kwenda na watoto wao sehemu za starehe na kuahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria wazazi watakaokaidi agizo hilo.
Katika hatua nyingine mwenyekiti huyo ameyataka baadhi ya makanisa yanayopiga muziki kwa sauti ya juu kuacha mara moja, kwa kuwa yanapelekea usumbufu kwa wakazi wanaoishi karibu na makanisa hayo.
Mhudumu wa afya ngazi ya jamii Raheli Faustine amesema kuwa watoto wengi wamekuwa wakikutana nao kwenye baa wakati wakitoa elimu ya kujikinga na ugonjwa wa kipindupindu hali ambayo inahatarisha maadili ya watoto.
Nao baadhi ya wananchi wa mtaa huo wameiomba serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria wazazi watakaobainika kwenda na watoto baa kwa kuwa ni chanzo cha mmomonyoko wa maadili kwa watoto.
Naye Shekhe wa wilaya ya Sengerema ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya Amani wilayani humo Shekhe Ahmad Jah amekemea tabia hiyo kwani inaharibu maadili ya watoto.
Aidha suala la baadhi ya wazazi kwenda na watoto sehemu za starehe limeshika kasi wilayani Sengerema licha ya Sheria ya mtoto ya mwaka 2009 kuzuia jambo hilo.