Sengerema FM

TANESCO wakata umeme chanzo cha maji Sengerema

3 July 2023, 12:29 pm

Picha ya bomba la maji: kutoka Maktaba

Kutokana na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Sengerema SEUWASA kukabiliwa na malimbikizo ya deni la umeme kiasi cha shilingi milioni mia tatu, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limekata huduma ya umeme katika chanzo cha maji kilichopo Nyamazugo.

Na: Emmanuel Twimanye

Wananchi mjini Sengerema mkoani Mwanza wamelazimika kutumia maji  yasiyo safi na salama  baada ya shirika la umeme Tanzania (TANESCO)  wilayani  humo kukata umeme kwa siku nne  katika chanzo kikuu cha maji cha  Nyamazugo  kwa madai ya kushinikiza Wizara ya Maji  kuwalipa deni lao la nyuma zaidi ya shilingi milioni mia tatu.  

Wakizungumza na Radio Sengerema baadhi ya wananchi wamesema kuwa kwa sasa wanapata usumbufu mkubwa  pindi wanapohitaji huduma muhimu ya maji.  

Mbunge wa jimbo la Sengerema Mh. Hamis Tabasam amesikitishwa na  wananchi kukatiwa huduma ya maji na kusema kuwa kwa sasa yupo jijini Dodoma kwa ajili ya kuzungumza na mamlaka husika ili kurejesha huduma hiyo.

Meneja utawala na  rasilimali watu wa SEUWASA  amekiri kukatiwa umeme na Tanesco katika chanzo cha maji na kwamba wanaendelea kuwasiliana na mamlaka za juu za kiutawala ili kutatua changamoto hiyo.

Hata hivyo  meneja wa Tanesco wilayani Sengerema Martine Kilenga  alipotafutwa na Radio Sengerema mara  kadhaa  ili kutolea ufafanuzi sakata hilo simu yake iliita bila kupokelewa.

Aidha tatizo la mji wa Sengerema kukatiwa umeme na wananachi  kukosa huduma ya maji limekuwa likijitokeza mara kwa mara ambapo mpaka sasa halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu na mamlaka husika .

Sauti ya mwandishi wetu Emmanuel Twimanye akiripoti taarifa ya upungufu wa maji mjini Sengerema