Sengerema FM
Sengerema FM
13 June 2026, 4:43 pm

Vishoka wawatapeli wananchi wakidai kuwaunganishia umeme maeneo ya vijijini Sengerema.
Na, Emmanuel Twimanye
Watu watatu wamekamatwa katika kijiji cha Busulwangili, Kata ya Tabaruka, wilayani Sengerema mkoani Mwanza, kwa tuhuma za kuwatapeli fedha wananchi kwa lengo la kuwaunganishia umeme majumbani.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Boniventura Kumogola, amesema watuhumiwa walimpigia simu wakimuulizia kuhusu mradi wa umeme katika vitongoji vya Chabakari na Stoo, kisha kufika ofisini na kujiandikisha kwenye daftari la wageni kabla ya kuanza kuwachangisha wananchi fedha kwa madai ya kuwaunganishia huduma ya umeme.
Baadhi ya wanannchi wanaodaiwa kutapeliwa fedha zao wamesikitishwa na tukio hilo na kuiomba serikali kuwachukulia watuhumiwa hatua kali za kisheria ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo huku baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wakimpongeza diwani wa kata hiyo kwa kusaidia kuokoa fedha zao .
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Chabakari A, Lucas Lazaro, amesema kuwa licha ya kukamatwa, watuhumiwa hao tayari walikuwa wamekwishakusanya fedha kutoka kwa baadhi ya wananchi kwa madai ya kuwaunganishia huduma hiyo.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa kijiji cha Busulwangili,Elia Chacha, amesema baada ya kutokea tukio hilo alipigiwa simu na Diwani wa Kata ya Tabaruka, jambo lililowezesha kuchukuliwa hatua za haraka na kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao.
Naye Diwani wa Kata ya Tabaruka, Sospeter Busumabu, ameagiza fedha zote zilizochukuliwa kutoka kwa wananchi zirudishwe na watuhumiwa hao wafikishwe kwenye vyombo vya dola kwa hatua zaidi za kisheria.
Majina ya watuhumiwa waliokuwa wamejiandikisha kwenye daftari la wageni katika ofisi ya serikali ya kijiji hicho ni Francisco John Wape , Joshua Mawazo na John Boniphace.