Sengerema FM
Sengerema FM
23 May 2026, 3:29 pm

Kutokana na ongezeko la vijana kujihusisha na vitendo vya kihalifu ikiwemo wizi,Vijana wilayani Sengerema wametakiwa kufanya kazi za kuwaingizia kipato halali ili kujikimu kimaisha.
Na,Emmanuel Twimanye
Mama mmoja aliyefahamika kwa jina la Yeneza Gulai mkazi wa Mtaa wa Misheni wilayani Sengerema Mkoani Mwanza amelazimika kumfikisha kijana wake Aman Ncheye (27) katika ofisi ya serikali ya mtaa huo baada ya kuchoshwa na tabia ya wizi inayofanywa na kijana huyo.
Akizungumzia tukio hilo, mama huyo amesema mbali na kujihusisha na vitendo vya wizi, kijana huyo pia amekuwa akimshambulia kwa kutumia kisu pamoja na kumung’ata sehemu mbalimbali za mwili wake, licha ya kumuonya mara kadhaa kuachana na vitendo hivyo, kijana wake ameendelea kujihusisha na wizi, hali iliyomlazimu kumfikisha katika ofisi ya serikali ya mtaa kwa ajili ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
Kwa upande wake, kijana huyo akiwa chini ya uangalizi wa serikali ya mtaa, amekana tuhuma hizo huku akimuomba radhi mama yake.
Baadhi ya wananchi wa eneo hilo wamewataka vijana kuachana na vitendo vya wizi ili kuepuka kuhatarisha maisha yao.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Misheni, Joseph Protas, amekiri kuwa kijana huyo amekuwa akijihusisha na vitendo vya wizi na kueleza kuwa wanatarajia kumfikisha kwenye vyombo vya dola kwa hatua zaidi za kisheria.
Naye Kamanda wa Polisi Jamii wa kata hiyo, Rajabu Tunge, amethibitisha kukamatwa kwa kijana huyo na kutoa wito kwa vijana kuachana na vitendo vya wizi na kujikita katika shughuli halali za kujipatia kipato.