Sengerema FM
Sengerema FM
27 May 2026, 5:04 pm

Kufuatia kukithili kwa baadhi ya wanawake kuwafanyia vitendo vya ukatili waume zao, Jeshi la polisi wilayani Sengerema lawataka wananchi kutoa ushirikiano ili kukomesha vitendo hivyo.
Na,Emmanuel Twimanye
Kijana Simon Kashangele (24), mkazi wa Kitongoji cha Senta B, Kata ya Nyamizeze wilayani Sengerema, amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kudaiwa kumwagiwa maji ya moto na mke mdogo aliyefahamika kwa jina moja la Mama Ruth kwa madai ya wivu wa kimapenzi.
Akizungumzia tukio hilo, Simon amesema ugomvi ulianza baada ya kumtaka mke wake mdogo kuacha kuongea na kuchati na wanaume wengine, ndipo alipomwagiwa maji ya moto, kisha mwanamke huyo kutokomea kusikojulikana .
Baadhi ya ndugu na wananchi wa eneo hilo wamesikitishwa na tukio hilo na kuiomba serikali kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mwanamke huyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hiyo.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Senta B, Mnana Mzinza, amewataka wanawake kuacha vitendo vya ukatili dhidi ya wanaume zao na kusisitiza umuhimu wa kutatua migogoro ya kifamilia kwa njia ya amani.
Kwa upande wake, Mratibu wa Dawati la Jinsia na Watoto wilayani Sengerema, Mponela Malongo, amewaomba wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha mtuhumiwa anakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
