Sengerema FM

Mtoto wa miaka 3 afa maji wilayani Sengerema

16 October 2023, 2:18 pm

Picha ya bwawa alilozama mtoto akichota maji katika kijiji cha Nyamtelela. Picha na Emmanuel Twimanye

Ikumbukwe mwezi September watoto wanne walipoteza maisha kwa kuzama kwenye bwawa kata ya Katunguru na kufanya jumla ya watoto sita kufa maji maeneo tofauti tofauti wilayani Sengerema kwa mwaka huu 2023.

Na;Emmanuel Twimanye.

Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 3 amefariki Dunia baada ya kuzama kwenye bwawa la maji wakati akichota maji katika Kitongoji cha Kabingo Kijiji cha Nyamtelela Kata ya Katunguru Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.

Akizungumzia tukio hilo Mataba Nkanija babu aliyekuwa akimlea mtoto huyo  amesema kuwa walikwenda shambani na kuwaacha nyumbani watoto na baada ya muda mfupi mmoja kati ya wajukuu zake  alifika shambani na kumueleza kuwa Victoria Mhoja amefariki Dunia kwa kuzama bwawani.   

Baadhi ya ndugu na majirani wa familia hiyo wamepokea tukio hilo kwa masikitiko na kuiomba serikali ya kijiji kuweka uzio katika bwawa hilo ili kunusuru maisha ya watoto.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kabingo Onesmo Mahona amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa hilo ni tukio la pili kutokea katika kitongoji hicho .

Kufuatia tukio hilo  mwenyekiti wa kijiji cha Nyamtelela   Kulwa Shija amewatahadharisha wazazi kuwa makini na watoto wao ikiwa ni pamoja na kuacha kuwagiza kuchota maji katika  katika eneo hilo  wakati serikali ya kijiji  ikiendelea na mchakato wa kuweka uzio katika bwawa hilo . 

Hata hivyo Jeshi la polisi kituo cha Katunguru limefika eneo la tukio na kuruhusu  kufanyika  kwa  taratibu za mazishi .

Taarifa ya Mwandishi wetu Emmanuel Twimanye Ikifafanua zaidi