Sengerema FM
Sengerema FM
16 July 2026, 10:41 pm

Ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa madawati kwa Shule za Misingi katika Halmashauri ya Sengerema, Mgodi wa Dhahabu wa Sotta Mining Corporation Ltd umekabidhi madawati zaidi ya 900.
Na, Said Mahera
Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema imepokea madawati 977 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 78 yaliyotolewa na Kampuni ya Mgodi wa Sotta Mining Corporation Limited, ili kukabiliana na uhaba wa madawati katika shule za msingi.
Akisoma taarifa ya mradi huo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Bi. Habiba Omari, Afisa Mahusiano wa kampuni hiyo amesema mgodi unaendelea kutekeleza wajibu wake wa kurejesha kwa jamii. Ameongeza kuwa kampuni pia inaendelea na ujenzi wa madarasa mawili katika Shule ya Sekondari Lubungo, Kata ya Igalula, kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 52.
Akimwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu, Bw. Wilibad Bandola, ameishukuru kampuni hiyo kwa mchango wake na kuwataka walimu kuyatunza madawati hayo.
Naye mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Bw. Abeli Fadhili amewataka wakuu wa shule zilizopokea madawati hayo kuyatunza ili kusaidia kufikia lengo la kumaliza changamoto ya upungufu wa madawati wilayani humo.
Baadhi ya wakuu wa shule walionufaika wameishukuru Kampuni ya Sotta Mining Corporation Limited wakisema madawati hayo yataboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Mgodi wa Sotta Mining Corporation Limited umeendelea kutekeleza sera yake ya kurejesha kwa jamii kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo, hususan katika sekta za elimu, afya na miundombinu.