Sengerema FM

Polisi na Wananchi wafanya usafi jumamosi ya mwisho wa Mwezi

31 July 2026, 7:02 pm

Polisi Jamii Kata wa Misheni, Inspector Asha Mohamed, akiongoza zoezi la usafi, Picha na Peter Marlesa

Jeshi la polisi Nchini linazidi kujisogeza kwa wananchi kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii kwa kushirikiana nao ili kuongeza ushirikiano baina ya wananchi na jeshi hilo.

Na,Peter Marlesa

Jeshi la Polisi wilayani Sengerema mkoani Mwanza limesema kampeni mbalimbali za kijamii, zikiwemo za usafi wa mazingira, zimeendelea kuimarisha mahusiano mema kati ya jeshi hilo na wananchi, huku zikihamasisha ushirikiano katika kulinda usalama na maendeleo ya jamii.

Akizungumza na wakazi wa Kata ya Misheni baada ya zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika katika kata ya Misheni, Mkuu wa Kitengo cha Takangumu na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Sengerema, Procesius Richard Rweyendera, amesema mamlaka kwa kushirikiana na wananchi zimejipanga kuhakikisha usafi wa mazingira unakuwa sehemu ya utamaduni na urithi utakaorithishwa kwa vizazi vijavyo.

Sauti ya Mkuu wa Kitengo cha Takangumu na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Sengerema, Procesius Richard Rweyendera

Kwa upande wake, Polisi Kata wa Misheni, Inspector Asha Mohamed, amesema ukaribu unaoendelea kujengwa kati ya Jeshi la Polisi na wananchi unapaswa kutumiwa kama fursa ya kufichua vitendo vya uhalifu na kuwafichua wahalifu, hatua ambayo itasaidia kuendelea kudumisha amani na usalama wa nchi.

Sauti ya Polisi Jamii Kata wa Misheni, Inspector Asha Mohamed

Nao Kamishina wa Skauti Wilaya ya Sengerema, pamoja na baadhi ya skauti na wananchi walioshiriki zoezi hilo, wamepongeza juhudi za Jeshi la Polisi za kushiriki shughuli za kijamii, wakisema hatua hiyo imeongeza mshikamano, kuimarisha mahusiano mema na kujenga imani kati ya wananchi na vyombo vya dola.

Sauti ya Kamishina wa Skauti Wilaya ya Sengerema na wadau wa usafi Sengerema

Kampeni za usafi wa mazingira zinazofanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi katika Mji wa Sengerema zinalenga kuimarisha ushirikiano kati ya mamlaka na jamii, kuhamasisha usafi wa mazingira kuanzia ngazi ya familia, pamoja na kujenga mazingira salama na yenye afya kwa wananchi wote.