Sengerema FM
Sengerema FM
25 September 2026, 9:29 pm

Kufuatia kuokotwa kwa mtoto mchanga mwenye umri wa mwezi mmoja akiwa ametelekezwa kwenye mtaro wa maji mjini Sengerema,familia moja imejitolea kumlea mtoto huyo, huku jamii ikitakiwa kuacha tabia za kutoa mimba au kutelekeza watoto.
Na;Emmanuel Twimanye
Mkazi wa Mtaa wa Igogo, Kata ya Nyampulukano wilayani Sengerema mkoani Mwanza, Silas Bulugu, amekubali kumlea mtoto wa kiume mwenye umri wa mwezi mmoja, aliyekuwa ametupwa mtaroni na kuokolewa na wasamaria wema.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa mtoto huyo katika misa takatifu iliyofanyika nyumbani kwake, amesema ameamua kumlea mtoto huyo ili awe sehemu ya familia yake.
Zawadi Emmanuel, mbaye ni mke wa Silas amekubali mtoto huyo kuingia katika familia yao na yuko tayari kushirikiana na mume wake kumpa malezi na upendo, licha ya kuwa tayari wana watoto wao wengine watatu.
Baadhi ya wananchi wa mtaa huo wameipongeza familia hiyo kwa upendo wa kukubali kumlea mtoto huyo .
Kwa upande wake, Paroko wa Parokia ya Yesu Kristo Mfalme Sengerema Mjini, Padri Edson Nduha, amembatiza mtoto huyo na kumpa jina la Emmanuel, huku Silas Bulugu na mke wake Zawadi Emmanuel nao wakibatizwa pamoja na kubarikiwa ndoa yao ,huku akipongeza familia hiyo kwa uamuzi wa kumlea mtoto huyo.