Sengerema FM
Sengerema FM
17 November 2026, 8:26 pm

Kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha nchini kwa baadhi ya maeneo mashimo yamegeuka kuwa mabwawa ya maji yanayosababisha maafa ya watoto kutumbukia na kusababisha vifo, ambapo jamii imetakiwa kuwa makini na mashimo hayo.
Na Emmanuel Twimanye
Mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi nane amefariki Dunia baada ya kuzama katika dimbwi la maji eneo la Nyambinti A kitongoji cha Balatogwa Kata ya Mwabaluhi Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza .
Akizungumzia tukio hilo Baba mzazi wa mtoto huyo Stephano Chelehani amesema kuwa walikwenda shambani na mke wake na kumwacha mtoto huyo nyumbani na wenzake na baada ya muda mfupi alipata taarifa kutoka kwa jirani yake kuwa mtoto wake amezama katika dimbwi la maji .
Mama mzazi wa mtoto ,Happynes Kapaya amesikitishwa na tukio hilo na kusema kuwa licha ya jitihada za kumpelekea katika Zahanati ya Balatogwa kwa ajili ya kupata matibabu tayari alikuwa amefikwa na umauti.
Baadhi ya ndugu na majirani wa familia hiyo wamepokea tukio hilo kwa huzuni na masikitiko .
Kwa upande wake ,Mwenyekiti wa Kitongoji cha Balatogwa safari Shigemelo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wananchi kuwa makini na watoto hususani katika kipindi hiki cha mvua, huku akitoa pole kwa familia kwa kumpoteza mtoto huyo.