Malima aagiza kuboreshwa upatikanaji wa mbegu za Korosho na minazi.
23 June 2021, 4:59 pm
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Kigoma Malima amemuagiza afisa kilimo wa halmashauri ya wilaya ya Pangani kuandaa mikakati ya upatikanaji wa mbegu za mazao ya minazi na korosho ili kuboresha mazao hayo wilayani humo.
Malima ameyasema hayo katika kikao maalumu cha baraza Madiwani kwa ajili ya kujadili taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kwa ukaguzi wa hesabu za halmashauri ya wilaya ya Pangani kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.
Akitoa maagizo hayo malima amesema kuimarika kwa zao la minazi na korosho kutawezesha kuongeza mapato katika halmashauri ya wilaya ya Pangani hivyo kusaidia kupiga hatua kimaendeleo.
Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa huyo amewaagiza wakuu wa taasisi na watendaji katika idara mbalimbali za halmashauri ya wilaya hiyo kushirikiana vema na madiwani katika halmashauri hiyo ili kufanya kazi kwa pamoja na kuongeza ufanisi katika kazi.
Baada ya kuhitimishwa kwa kikao hicho Malima amekabidhi mifuko 1000 ya saruji na mabati 300 kutoka kwa mbunge wa jimbo la Pangani Mheshimiwa Jumaa Aweso ili kutimiza ahadi alizowahi kuzitoa.
Kilimo ni miongoni mwa sekta muhimu katika kuchangia mapato ya halmashauri ya wilaya ya Pangani huku zao la minazi likitajwa kushika nafasi ya pili kwa makusanyo nyuma ya zao la mkonge.