Ujenzi Kituo cha Polisi Mivumoni
13 April 2021, 1:41 pm
Kamishina wa Polisi Jamii Tanzania Mussa Ali Mussa amefanya ziara wilayani Pangani mkoani Tanga na kuweka jiwe la msingi katika kituo kidogo cha Polisi kilichopo kijiji cha Mivumonini wilayani humo.
Akizungumza wakati wa tukio la uwekaji jiwe kwa ajili ya Ujenzi wa kituo hicho kamishna Mussa ametanabaisha kuwa mabati ya kumalizia ujenzi huo yataletwa na kuwawaomba wananchi na viongozi kuendeleza juhudi hizo huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Askari kata ili kuleta Amani,utulivu na usalama kwa Raia wote..
“Lakini sisi kwa awamu ya mwanzo tunasema basi bati la jengo hili sisi tutalileta, pale tu tukishakuambiwa kunahitajiwa bati ngapi? Mia, Ishirini,Thelathini Hamsini, basi tuitazipitishia kwa uongozi wenu wa Polisi ili ziletwe wakati huo tunasubiri na mambo mengine ili tuone lakini kwa ujumla sisis tumefurahi na salamu zenu hizi nitazichukua nakuzifikisha kwa Mkuu wangu Afande IGP na nna hakika nay eye ataridhika na atafarijika kwa juhudi hizi mnazozichukua.”
Amesema Kamanda Mussa Ali Mussa
“Ninachowaomba tuendelee na juhudi hizi za kulijenga jengo hili hadi tuone linamalizika kwa jitihada zetu sote. Lakini na pale litakapomalizika basi ni lazima tushirikiane na hawa Askari ambao watakaokuwepo ili muweze kulifikia lile lengo ambalo ninyi mnalolitaka kwa sababu jengo ni kitu kingine na utendaji ni kitu kingine tunaweza tukawa na jengo zuri sana lakini ile kazi iliyokusudiwa isifanyike, lakini tukiyaunganisha mambo haya matatu jengo zuri lipo,askari wapo,na ninyi wenye nia ya kuona maeneo yanakuwa shwari na salama mpo,lile lengo litaweza kufanikiwa. Niwaombe tena tuendelee kushirikiana ili maeneo yetu haya yaweze kuwa shwari ili tuendelee na shughuli zetu za kijamii na za kiuchumi katika mazingira yaliyokuwa mazuri” (Amesema Kamishna Mussa A. Mussa)
Akisoma risala kwa Kamishna huyo kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho pamoja na viongozi Bwana JOHN JACKSON MPAZINGA amesema kuwa wananchi wamechangia kiasi cha shilingi milioni nne laki saba themanini nne elfu ambapo wameomba kuungwa mkono.
“Ndugu mgeni rasmi wananchi wa kijiji cha Mivumoni wameona umuhimu wa ulinzi na usalama makwao na raia jirani kwa Kata ya Madanga. Ujenzi wa kituo hiki unajengwa na nguvu za wananchi kwa gharama ya milioni ishirini na tano laki tatu themanini na tatu elfu mia tisa na ishirini- shilingi za kitanzania, kitu ambacho kinatuwia ugumu ni kumudu gharama ya ujenzi huo, hivyo uongozi wa kijiji unaomba serikali iwaunge mkono kwa ujenzi huu kwa fedha au vifaa vinavyoweza kukidhi sehemu iliyobaki ya ujenzi huu,”
Amesema Ndg Mpazinga
“Ndugu mgeni rasmi, katika ujenzi huu wananchi tayari wamechangia jumla ya shilingi milioni nne laki saba themanini na nne elfu shilingi za kitanzania hadi hapo jengo lilipofikia hivyo kuungwa mkono ni jambo la umuhimu. Uongozi wa kijiji unakutakia kila la heri kwa mchango wako utakaoweza kusadia Asante. (Amesema John Jackson Mpazinga)
Kwa upande wa baadhi ya wakinamama waishio kijijini hapo wamefurahi kuona ujio wa kiongozi huyo na kushukuru kituo hicho kujengwa katika kijiji chao kwa kuwa ni mkombozi na kwamba vitendo vya ukatili na unyanyasaji vitapungua.
“Sisi wakinamama tumefarijika sana kutembelewa na viongozi wakubwa wetu akiwemo kamisha wa Polisi jamii Tanzania imekuwa jambo la faraja.
Pia tunashukuru kwa hili jengo kujengewa hapa kijijini kwetu kwa kuwa uhalifu wote utapungua,vitendo vya ukatili vitapungua, unyanyasaji nao utapungua maana kituo hiki ni mkombozi wetu kwa sababu kwanza ukatili hapa kijijini kwetu ni mwingi, hapa kijijini kwetu pombe zinauzwa holela yani kiholela holela yani watoto wetu wanaharibiwa,kwa sisi wakinamama tulikuwa tunasikitika watoto wetu wanaharibikiwa lakini ufumbuzi wa kupatikana kituo cha Polisi kwa sisi wakinamama tumefurahia kwa sababu pombe hazitauzwa kiholela.
Pia tunaahidi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa ushahidi pale patakapotokea kitendo cha ukatili wa kijinsia yani tunalilia ujenzi wa kituo hiki hata kesho uishe na tunashukuru kwa ujio uliotufikia kwa kuahidi vitu na tunaimani kwamba watavitoa”. (Wakinamama)
Jeshi la Polisi wilayani Pangani limekuwa likishirikiana na wananchi katika ukarabati na ujenzi wa Vituo vya Polisi ili kuhakikisha kunakuwa na ushirikiano kwenye ulinzi shirikishi na hatimaye wananchi waishi kwa Amani na usalama katika kujipatia maendeleo ambapo awali walianza na ujenzi wa kituo kikuu cha Polisi Pangani mjini.