Daraja mto Pangani kuwa mwarobaini wa ajali kwenye kivuko cha MV Tanga
3 October 2024, 3:20 pm
Watu huvuka ng’ambo moja na nyingine ya mto Pangani kwa ajili ya mahitaji ya kibiashara,shughuli za uzalishaji mali, huduma za kiofisi kama vile ofisi ya halmashauri ya wilaya ya Pangani,huduma za kibenki,hospitali ya wilaya,soko kuu la mkoa Tangamano au stendi kuu ya mabasi kuelekea mikoa ya Jirani hivyo kufanya watu kuhitaji kuvuka kila siku iitwayo leo.
Na Rajabu Mrope
Muundo wa wilaya ya Pangani.Wilaya ya Pangani ina vijiji 33, na mto Pangani unagawa wilaya hii kwenye pande mbili upande mmoja ukiwa na idadi ya kata 8 na vijiji 22 na upande ng’ambo ya pili ukiwa na idadi ya kata 6 na vijiji 11.
Kumbukumbu mbalimbali ambazo hazijawahi kuripotiwa huko nyuma bali kutokana na simulizi za watu zinaonesha ajali mbalimbali zimewahi kuutokea kwenye kivuko cha MV Tanga zikihusisha magari ya abiria na binafsi.
Historia ambayo haikuandikwa.Mzee Abushiri Mohamed Mbaruku ni mzaliwa wa ng’ambo ya pili katika eneo linalofahamika kama Bweni,kwa sasa ana umri wa miaka 79 anasema mwaka 2006 basi aina ya SHAKILA,lilizama kwenye kivuko cha Mv Tanga,na wakati huo ndio ambao sheria ya abiria kushuka kwenye kabla ya gari kuingia kivuko ilipoanza kutumika.
“nakumbuka mwaka huo nikiwa hapa majira ya asubuhi basi hili lilitumukia mtoni,nahisi dereva alipoteza maisha wengine waliokolewa na wengine walipoteza maisha ila sikumbuki vizuri,unajua wakati ule hata vyombo vya Habari huku kwetu Pangani hamna ila kwa uchache ninayokumbuka ndio hayo’’
Taarifa zilizowahi kutangazwa.
Tukio la kwanza.
Gari moja aina ya MITSUBISH-CANTER yenye namba za usajili T 336 AAE mali ya Bwana MRISHO HEMEDI BAKARI, limeacha njia na kutumbukia katika Mto Pangani eneo la CASTAM palipo na Bandari ya Pangani.
Akithibitisha tukio hilo Mkuu wa Polisi Wilaya ya Pangani Bi Christina Musiani amesema kuwa tukio hilo limetokea leo Desemba Mosi 2017 majira ya saa Tano na Nusu Asubuhi, baada ya kondakta wa gari hilo Ally Hemedi mwenye umri wa miaka 23 alipokuwa akiligeuza gari hilo mara baada ya kumaliza kupakua Machungwa waliyokuja nayo kutoka Wilayani Muheza.
Aidha Mkuu huyo wa Polisi Pangani amesema kuwa pamoja na ajali hiyo kutosababisha madhara yoyote kwa Binaadamu, imesababisha uharibifu wa gari hiyo huku kijana Ally Hemedi ambaye ni Kondakta wa gari hilo akitokomea kusipojulikana hadi sasa.
“Pamoja na kusababisha uharibufu katika gari hilo tunashukuru Mwenyezi Mungu ajali hiyo haikusababisha madhara yoyote kwa binaadamu, tayari gari hiyo imeshatolewa na iko kituoni kukaguliwa na taratibu nyingine za kisheria zinaendelea, na kijana Ally Hemedi ambaye ni Kondakta wa gari hilo ametoroka hatujui amekimbilia wapi hadi sasa’
amesema Mkuu wa Polisi Pangani Bi Christina Musiani.Source: – Pangani fm BlogLink:- https://panganifm255.blogspot.com/2017/12/gari-kuacha-njia-na-kutumbukia-mto.html
Tukio la Pili.
Siku ya Jumapili, Tarehe 23/07/2023 majira ya saa sita za mchana, kumetokea ajali katika eneo la Pangani ambapo kivuko cha MV. TANGA na MV. PANGANI II vinatoa huduma kati ya Pangani na Bweni Wilayani Pangani Mkoani Tanga baada ya Basi la abiria linalotambulika kwa jina la MOA linalofanya safari zake kutoka Tanga mjini kupitia Pangani na kuvuka kwenye kivuko hadi Kipumbwi kuzama baada ya kufika upande wa Bweni lilipokuwa likivuka kutokea upande wa Pangani Kuelekea Bweni.
Akizungumza eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Pangani Bi. Zainab Abdallah ambaye alifika eneo la tukio mara baada ya ajali hiyo kutokea, amesema kuwa hakuna yeyote aliyepoteza maisha wala majeruhi kwenye ajali husika kwakuwa Basi hilo lilikwisha toka kwenye eneo la kivuko na kwa bahati mbaya lilizimika likiwa nje ya gati, dereva alijitahidi kuliwasha tena ili kuliondoa lakini alishindwa kulimudu kwakuwa eneo hilo ni la muinuko na Basi hilo kurudi kinyume nyume na kutumbukia kwenye maji.
Dereva wa Basi hilo aliruka na kujiokoa.”Basi la Kampuni ya MOA ambalo lilitumbukia majini likiwa linatoka ndani ya kivuko kwenda nchi kavu Pangani tayari limetolewa kwenye maji, nawapa pole wana Pangani na Watanzania kwa taharuki na tunafuatilia ili matukio kama haya yasijirudie tena.” Amesema Bi Zainab.
Hakukuwa na majeruhi yoyote aliyeripotiwa kutoka kwenye ajali hiyo kwakuwa abiria wote walikuwa tayari wameshushwa kutoka kwenye Basi husika kama ambavyo sheria za usalama wa vivuko zinaagiza, vilevile abiria huanza kushuka kwanza kutoka kwenye kivuko kabla ya magari kuruhusiwa kuanza kutoka.
Source :-Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA)Kauli ya TEMESA.
TEMESA inaendelea kuwasisitizia abiria kufuata maelekezo ya usalama yanayotolewa na mabaharia wakati wote wanapotumia vivuko na inatoa pole kwa wahusika wa Basi lililopata ajali lakini pia inawakumbusha wamiliki wa magari kuhakikisha magari yao yanakua katika hali bora wakati wote ili kuepusha ajali zinazoepukika.
Ahueni yaja.Serikali Imeanza Ujenzi wa Daraja Kubwa la Mto Pangani Lenye Urefu wa Mita 550 Litakalo gharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 82.19 utakaokamilika ndani ya Miezi 36 ukijumuisha pamoja na Ujenzi wa Kipande cha Barabara yenye urefu wa Kilomita 14 za Kiwango cha Lami kutoka Bweni Mpaka Tungamaa.
Nini kauli za wananchi?
Wanafunzi.
Baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika shule ya sekondari Kilimangwido ambayo inapatikana upande wa pili wa mto wamesema,mbali na ajali ila pia Daraja hilo litawasaidia kuvuka kwa wakati tofauti na sasa hivi wanaposubiri kivuko ambacho huwa kinachukua si chini ya dakika 15 hadi kivuko hiko kijae.
’’sisi wenyewe hapa kuna wakati tunachelewa shule tunaadhibiwa,ila kama kungekuwa na Daraja tungevuka haraka na kuwahi,na pia sula la suala la usalama kuna wakati kunatokea msongamano wa kugombea kuvuka watu wanapokuwa wengi inaweza hatari kwetu na kivuko kinatumika kimoja tu”
Mhusika mwengine.Bwana Matteo Moris ni mfanyabiashara wa mboga mboga kutoka Kijiji cha Kikokwe hapa anaelezea mkwamo wa kibiashara na matukio yaliyowahi kutokea yanayohatarisha usalama.
‘’Kuna wakati nafika pale Bweni kivuko kimeharibika ikabidi nivuke na ngalawa,hali ambayo mimi sikuona kuwa ni salama ila sikuwa na namna kwa sababu mboga zangu zingeharibika” amesema Matteo Moris.‘’
Kuna wakati pia kivuko kimeharibika Katikati ya maji kikawa kama kinaelekea upande huu (akionesha upande ambao ndio kunajengwa Daraja sasa hivi) hadi baadae kuna fundi akaja na boti wakarekebisha hali ikakaa sawa’’
Ziara ya Mbarawa.
Mhe. Prof. Makame Mbarawa,Waziri wa ujenzi na uchukuzi, alifanya ziara ya kukagua ujenzi wa daraja la muda la mto Pangani, Agosti 28,2023.
Prof. Makame aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Pangani Mhe Zainab Abdallah, Waziri wa Maji (mb) wa jimbo la Pangani mhe Jumaa Aweso,na viongozi wengine.
Prof. Makame amepongeza juhudi za ujenzi wa daraja hilo la muda, ambalo limekamilika kwa 100% na tayari kwa kuanza ujenzi wa daraja la kudumu.
“Niwaombe wakandarasi wajenge daraja lenye ubora na viwango vya juu,ili liweze kutoa huduma yenye tija kwa Taifa letu la Tanzania”.
Awali akisoma utekelezaji wa ujenzi wa daraja hilo mradi unaotekelezwa na kampuni ya Ms Shandong Luqiua Group ya Kichina, Mhandisi wa Tanroad Mhandisi Safia Maliki Alisema serikali itaigharamia mradi huo kwa asilimia 11.16 na benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) itatoa fedha kwa asilimia 88.84.
‘’Daraja hili litakapokamilika litarahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali zq kijamii, huku pia likichochea uchumi kwa wananchi kufanya shughuli za kibiashara kwa uhuru na gharama nafuu zaidi’’.Jumaa Aweso Waziri wa maji ambae pia ni mbunge wa Jimbo la Pangani,alizungumza wakati wa ziara hiyo akiwa amembatana na Profesa Mbarawa akikagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja hilo.Matarajio ya wananchi.‘’Mimi nafikiri Daraja likikamilika basi kila kitu kitakuwa sawa,hakutakuwa na kuchelewa kusubiri kivuko wala kuogopa hatari yoyote ambayo inaweza kujitokeza pale kivuko kinapokuwa kimegaribika’’ Mwanaisha Rashid mkazi wa eneo la Bweni.Mpango wa serikali.Bajeti wizara ya ujenzi.Mei 29,2024 Waziri Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa aliwasilisha makadirio ya bajeti ya kiasi cha, Sh bilioni 81.4 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh. Trilioni 1.6 kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2024/25.Katika muhtasari wa hotuba ya Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa (mb), akiwasilisha bungeni mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2024/25 aliyoitoa mwezi Mei mwaka huu inaonesha hadi mwezi huo Daraja la Pangani ujenzi wake ulikuwa 23%.