Vijana tafuteni kipato cha halali, serikali ipo nanyi
6 May 2024, 7:36 am
Mnapofanya kazi zenu kwa uhalali serikali inawaona na itawawezesha kukabiliana na changamoto mnazokutana nazo.
Na Cosmas Clement
Vijana mkoani Tanga wametakiwa kujituma kwa kufanya kazi halali za kujiingizia kipato ili kuwawezesha kusonga mbele kimaendeleo na kupunguza tatizo la vijana kukosa ajira.
Hayo yamesemwa Jumapili May 5, 2024 na Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) MNEC Ndugu Rajabu Abdulrahman wakati akizindua Shina la wakereketwa wa CCM Mgandini jijini Tanga ambalo lina vijana wanaojihusisha na biashara za nyama na ufundi gereji.
Akizungumza katika uzinduzi huo Ndugu Rajabu amesema vijana wanapaswa kujituma kwakuwa serikali ipo kwa ajili ya kuwajengea miundombunu mizuri itakayowawezesha kujiajiri huku akitoa kiasi cha shilingi milioni mbili na laki tano kwa shina la wauza nyama na mafundi gereji Ngamiani.
Akiwa katika Shina la wakereketwa Machinga na Bodaboda Barabara ya 9 Ndugu Rajabu ametoa kiasi cha shilingi milioni Mbili huku akiahidi kuendelea kuwakumbusha viongozi mbalimbali kuwawezesha kutatua changamoto zinazowakabili.
Awali katika risala ya shina la wakereketwa wa CCM Mngandini, imebainisha kuwa pamoja na kujiajiri bado umoja wao unakabiliwa na changamoto katika shughuli zao ikiwemo vifaa duni vya kufanyia kazi.
Hayo yanajiri wakati Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi mkoani Tanga Bwana Rajabu Abdulraham akifanya ziara ya kichama jijini Tanga huku akihamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2024.