Pangani FM
Pangani FM
27 November 2025, 5:36 pm

Zamani tulikuwa hatufuatilii utabiri wa hali ya hewa, wakati mvua zinanyesha sisi tunaandaa mashamba , mvua ikikata sisi tunapanda matokeo yake mbegu zashambuliwa na wadudu lakini sasa hivi tunafuatilia utabiri na tunavuna vizuri, ahsanteni CAN TZ.
Na Cosmas Clement
Elimu ya Matumizi ya utabiri wa jadi wa hali ya hewa kwa njia ya jadi inayotolewa na shirika la CAN TZ imetajwa kuleta tija kwa wanajamii wa vijiji vya Mivumoni na Msaraza kwa kupata mavuno ya uhakika kwa wakulima na wafugaji.
Hayo yamezungumzwa na Wajumbe wa kamati za huduma za utabiri wa hali ya hewa kwa njia ya jadi katka kikao cha tathimini kilichoendeshwa na shirika la CAN TZ.
Wakizungumza katika kikao hicho Bi Ana Manga na Adam Julius ambao ni watabiri wa hali ya hewa kwa njia ya Jadi kutoka kijiji cha Mivumoni wamesema kutokana na elimu hiyo walioipata wamefanikiwa kutoa elimu kwa wakazi wa vijiji vyao na kupelekea kuwa na mavuno yenye tija.
Nao wakulima kutoka vijiji vya Msaraza na Mivumoni ambao ni wanufaika wa elimu hiyo wamesema kutokana na elimu aliyopatiwa na watabiri hao ameweza kuendesha kilimo kwa manufaa tofauti na hapo awali.
Kwa upande wa maafisa ugani kutoka idara ya kilimo mifugo na uvuvi halmashauri ya wilaya ya Pangani wamesema uwepo wa elimu hiyo inayotolewa na Shirika la CAN TZ imewarahisishia katika utendaji kazi zao za kuwafikia wanajamii.
Bwana Boniventure Mchomvu Mkuu wa Program na Meneja wa uendeshaji kutoka shirika la CAN Tanzania amesema ni muhimu kwa jamii za wakulima na wafugaji na wavuvi kutumia utabiri wa hali ya hewa kwa kuendesha shughuli zao kwa tija.