Pangani FM
Pangani FM
8 June 2025, 7:08 pm

‘Sisi tuna uzoefu wa minada ya korosho hapa Tanga lakini baadae korosho zikawa zinatoroshwa kwenda nje ya mkoa wetu, ni kwa sababu tulifanya mnada mara moja haukuendelea.’
Na Cosmas Clement
Mkuu wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Buriani leo amezindua mnada wa ufuta katika kijiji cha Stahabu wilayani Pangani ambapo tani zipatazo tano 122.6 za wakulima zinatarajiwa kuuzwa siku ya jumatatu ya tarehe 9/6/2025.
Akizungumza katika uzinduzi wa mnada Dkt Batilda amewaasa wakulima kukusanya mazao yao katika mifumo rasmi ya ushirika ili kupata manufaa kiuchumi akiahidi kuhakikisha minada hiyo inakuwa endelevu.
Mrajisi wa vyama vya Ushirika mkoa wa Tanga Bwana John Henjewele amesema kuzinduliwa kwa mnada huo kutawezesha kutangaza fursa ya uwepo mazao ya ufuta na kuimarisha minada ya mara kwa mara.
Naye mkuu wa wilaya ya Pangani Mhe Gift Msuya amesema kuwa uwepo wa mfumo wa uuzaji wa mazao mchanganyiko kupitia mnada utasaidia kuondoa matapeli.
Kwa upande wake Bwana Gread Saidi afisa kilimo kutoka mamlaka ya udhibiti wa Nafaka na mazao mchanganyiko COPRA amezishauri Halmashauri kudhibiti mipaka ili kuia utoroshaji wa mazao nje ya mkoa.
Uzinduzi wa mnada wa ufuta umefanyika katika ghala la Stahabu kupitia AMCOS ya MITUMWE.