

15 February 2025, 9:40 pm
Pamoja na kwamba alipokonywa bakuli lenye sumu aliyoiandaa ili ajiue, lakini alifanikiwa kujiua kwa kutumia shuka.
Na Hamisi Makungu
Kijana mmoja aliyetambulika kwa majina ya Charles Yacobo Yohana mwenye umri wa miaka 30 mkazi wa Kijiji cha Mindu Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga adaiwa kujinyonga baada ya kunusurika katika jaribio la kunywa sumu usiku wa kuamkia leo Jumamosi.
Kwa mujibu wa mama mzazi wa marehemu Bi. Halima Hassani Mzee, kijana huyo amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya akili tangu mwaka 2010, ambapo kwa nyakati tofauti amekuwa akijaribu kutaka kujitoa uhai kwa kunywa sumu.
Hata hivyo jana Ijumaa mama huyo alimkuta kijana wake anakoroga sumu ya panya kwenye bakuli, na baada ya kufanikiwa kumnyang’anya, kijana huyo aliondoka nyumbani akiwa na mfuko ambao ndani yake kulikuwa na shuka aliyoitumia kujinyonga.
Kwa upande wake baba mdogo wa marehemu Bwana Dastan Rafael amesema mbali na kusumbuliwa na ugonjwa wa akili kijana huyo alikuwa akipata nafuu anafanya shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato.
Nao baadhi ya ndugu na marafiki wa karibu wa marehemu wamesimulia machungu ya kuondokewa na mpendwa wao ambaye hali yake ilianza kubadilika mara baada ya kuanza kuugua maradhi ya akili.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mindu Bwana Bakari Zuberi Kilango amethibitisha kutokea kwa tukio hilo kijiji kwake, na kwamba taarifa za tukio hilo alizipata kutoka kwa wananchi.
Mpaka taarifa hii inaruka hewani Polisi Wilaya ya Muheza imesema haina mamlaka ya kuzungumzia tukio hilo, na kwamba kinachofanyika kwa sasa ni kukamilisha ripoti baada ya kutoka eneo la tukio kwa ajili ya kuituma kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga.