Uvuvi wa dagaa chachu biashara Tanzania, DRC
27 October 2024, 11:00 am
Kwa sasa uvuvi wa dagaa aina ya uono kwenye Bahari ya Hindi ni uvuvi maarufu Tanzania hivyo kuvutia wafanyabiasha kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuongeza mapato kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Na Rajabu Mrope
Eneo la Uvuvi Tanzania.
Maziwa makuu.
Eneo la maji baridi linajumuisha maziwa makuu matatu ambayo ni Ziwa Victoria lenye ukubwa wa kilometa za mraba 68,800 ambapo Tanzania humiliki kilometa za mraba 35,088 (51%); Ziwa Tanganyika lenye kilometa za mraba 32,900 ambapo Tanzania humiliki kilometa za mraba 13,489 (41%) na Ziwa Nyasa lenye kilometa za mraba 30,800 na Tanzania humiliki kilometa za mraba 5,760 (18.51%).
Eneo la Bahari.
Eneo la Bahari limegawanyika katika Maji ya Kitaifa (Territorial Sea) yenye ukubwa wa kilometa za mraba 64,000 na Ukanda wa Uchumi wa Bahari (Exclusive Economic Zone – EEZ) wenye ukubwa wa kilometa za mraba wa 223,000.
Vilevile, Tanzania Bara ina Ukanda wa Pwani wenye urefu wa kilometa 1,424 (kutoka mpakani mwa Nchi ya Kenya kwa upande wa Kaskazini na Nchi ya Msumbiji kwa upande wa Kusini).
Mnufaika mmoja mmoja.
Mbebaji wa Dagaa wabichi.
Hawa wanahusika na kubeba uono mbichi kutoka kwenye maji hadi kwenye eneo maalumu kwa kuchemshia,hulipwa kati ya shilingi elfu 1500 hadi 4000 hadi eneo husika kutokana na umbali kwa dagaa wanaojaa ndoo mbili za maji za lita 20.
Saumu Mbezi mkazi wa Kipumbwi anasimulia anavyolea familia yake kwa kazi,’’nina mwaka wa 8 kwenye kazi hii inanisaidia kupeleka Watoto wangu shule,japo kuna wakati inatakiwa upumzike kwa sababu inaumiza kifua,mpango wangu siku moja nimiliki biashara ili nipumzike ila kwa sasa imeisaidia sana’’
Wafanyabiashara.
Daud Pandu,kutoka kata ya Kigombe wilayani Muheza anasema wakati wa uvuvi wa dagaa wavuvi wanaokuja kukaa rago inawasaida wao kufanya biahara zaidi,’’kwa mfano hapa mimi ninauza vyakua,vinywaji,sasa zile wiki mbili za mavuvi huwa nauza sana yani tunatamani uvuvi huu uwe moja kwa moja ila ndio hivyo kuna wiki mbili za kuvua na wiki mbili za mpandisho (siku ambazo zio za mavuvi)”
Uvuvi wa dagaa hutumia taa aina za karabai,ambazo wakati wa giza ndio humulika mbali zaid,dagaa wanapofuata mwanga huo wa taa hubakia kwenye nyavu,kutojua kwao ndio fahari na furaha ya mvuvi.
Inapofika kipindi cha mwezi kuwaka wavuvi wanaovua dagaa usiku hupumzika na kusubiri kipindi kingine cha giza ambacho huita,Bamvua.
Wachemshaji.
Hawa hupatiwa fedha na wafanyabiashara kutoka Kongo kwa ajili ya kununua dagaa na kuchemsha,kisha wao baadae kuchukua dagaa wakavu kwa bei watakayokubaliana.
Na hapa Bi Shakila Mgeni kutoka Kata ya Mkwaja wilayani Pangani akizungumza na makala hii,anasema katika kipindi cha miaka 5 cha kazi yake amefanikiwa kujenga nyumba yake,kwani amejiingiza kwenye kazi yake hiyo mara tu baada ya kupoteza mumewe mwaka 2020.
‘’Mimi nina kazi hii tangu nifiwe na mume wangu tulikuwa tunamiliki kiwanja tu,ila nashukuru sasa hivi nimejenga kibanda japo cha tope,juu bati zangu chache Maisha yanaendelea,utasema nikae Mungu nipe,atakupa kidonda ushunge nzi”
Wauza migahawa.
Mama Husnah Mohamed kutoka Kipumbwi Pangani,anasema wakati wa wiki 2 za uvuvi anapata si chini ya kiasi cha shilingi million 1 na zaidi ambayo ni faida ya kulipa wafanyakazi alionao,pesa ya kununua unga wa ngano,mafuta na sukari.
‘’Mimi hapa nauza chai asubuhi,chakula mchana na jioni na nina watu maalumu ambao wanaweka oda,ambazo nawapikia chakula wanakula kabla ya Kwenda baharini,hivyo nikitoka nyumbani asubuhi narudi nyumbani usiku” Ameongeza Mama Husnah Mohamed kutoka Kipumbwi wakati akizungumza na makala hii’’
Mfanyabiashara wa ndani.
John Simon yeye anasafirisha dagaa kupeleka Mkoani Arusha,ambapo anasema bei huko ni nzuri ukitoa gharama za usafirishaji ushuru na mambo mengine muhimu pale anaposafiri.
‘’ Kwa sasa gunia moja la dagaa kwa sasa linauzwa kati ya Sh120,000 hadi Sh130, 000 kulingana na ubora,ambapo kwa gunia la dagaa la kilo 100 ni wastani shilingi 1200 hadi 1300,sasa kule Arusha kilo moja ya dagaa inafika hadi shilingi 10000 hadi 12,000 kwa rejareja hivyo kila kilo unapata faida kama 8700 hadi 8800 hapo ukitoa ushuru na usafiri,umekula njiani kidogo waweza kubaki nakama elfu 4000,ambapo kwenye kila gunia unaweza kupata kama shilingi 400 000 kwa gunia,hivyo msimu wa uvuvi ukiwa mzuri bei huku ikishuka na faida kule inaongezeka zaidi ya hapo”
Mfanyabiashara wa Nje.
Juma Masud mfanyabiashara anayesafirisha bidhaa hiyo Kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliiambia makala hii kwamba, ‘’yaani kule Congo dagaa inasaminiwa sanaa kuliko kawaida ni sawa na chipsi kwa wadada Bongo kule mpaka unga wa dagaa upo wanatengenezea uji.
Kwa ufupi dagaa inaliwa kwa haraka sana na faida ni kubwa kwa mfano gunia iliyo nunuliwa kwa 200000/= kule inaweza kuuzwa kuanzia 600000/= na kuendelea’’
Juma Masud anasema ili ufanye biashara vizuri kuna utararatibu lazima uufuate, uwe na tin namba na leseni ya biashara kutoka TRA na hiyo leseni ya TRA uwe na leseni ya kusafirishia dagaa ndani ya tanzania ambayo kwa sasa ni elfu 30 pia uwe na kibali kutoka wizara husika ya mali asili ambacho ukifuatilia huwa vinatoka dodoma kwenye wizara husika.
Mapato ya uvuvi wa dagaa kwa halmshauri ya wilaya ya Pangani
Kwa mujibu wa Afisa uvuvi wilayani Pangani,Bwana Joseph Mabagala amesema kwa sasa ushuru ambao halmshauri inakusanya kutoka kwa wachuuzi wa dagaa ni shilingi elfu kwa guni la kilo 100 ambalo limeshashindiwa kwa ajili ya kusafirishwa ndani ya nchi.
‘’Kwa guni la kilo 100 huwa linatozwa shilingi elfu 20,lakini pia tunapata mapato kutokana na leseni ya uvuvi ambayo huwa ni shilingi elfu 30 kwa mwaka, Leseni zote za uvuvi Tanzania Bara zinatolewa chini ya Sheria ya uvuvi Na.22 ya mwaka 2003 na Kanuni zauvuvi za mwaka 2009 (G.N. Na. 308 ya 28/8/2009). Leseni za uvuvi hutolewa kwa mujibu wa sheria na kanuni za uvuvi kama ifuatavyo, leseni za vyombo vya uvuvi , leseni za kujishughulisha na biashara ya kuuza mazao ya uvuvi’’ametanabaisha Joseph Mabagala Afisa Uvuvi wilayani Pangani.
Pato la Uvuvi wa Dagaa Jiji la Tanga.
Sheria Ndogo za(Ushuru wa Mazao ya Uvuvi) za Halmashauri ya Jiji la Tanga zilizotungwa mwaka 2019. Tangazo la Serikali Na. 209
AINA YA USHURU
KIWANGO CHA USHURU
Chini ya kilo 50.
Shilingi elfu 5000 kwa gunia.
Kuanzia kilo 51 hadi kilo 100.
Shilingi elfu 10,000 kwa gunia.
Kuanzia kilo 101 kuendelea.
Shilini elfu 15,000 kwa gunia.
Source :- Halmshauri ya Jiji la Tanga.
Pato la nchi.
Uzalishaji wa Daga ana thamani yake.
Takwimu za wizara ya Uvuvi Zanzibar za mwaka 2023 zinaonesha uzalishaji wa dagaa
umeongezeka kutoka tani 2,405 zenye thamani ya shilingi bilioni 10.33 hadi tani
21,827 zenye thamani ya shilingi bilioni 89.31 kutoka mwaka 2020.
MUHIMU:-Hili ni ongezeko la tani 19422 kwa kipindi cha miaka 4 abapo ni sawana tani,4855 kwa mwaka,tani 404 kwa mwezi,na tani 13 kwa siku,na ni sawa pia na kilo 309 kwa kila saa moja.
Hii iliongeza kutoka thamani ya shilingi billion 10.33 hadi billion 89.31.kwa kipindi cha miaka 4, ambapo ni sawa na ongezeko la billion 19.75 kwa mwaka,billion 1.6 kwa mwezi,na million 53.3 kwa siku na kila saa moja nchi iliingiza jumla ya shilingi million 2.2.
Usafirishaji wa Daga na thamani yake.
Usafirishaji wa dagaa umeongezeka kutoka tani 3,579 zenye thamani ya shilingi bilioni 12.31
mwaka 2020, hadi kufikia wastani wa tani 9000 zenye thamani ya milioni 35 kwa
mwaka 2023.
Ushirikiano wa Kiuchumi Tanzania na Congo DR.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa nchini Tanzania ya mwaka 2020, nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ndio inayoshika nafasi ya kwanza miongoni mwa nchi jirani kupitisha mizigo katika bandari ya Dar es Salaam, DR Congo hupitisha zaidi ya 30% ya mizigo yote.
Mbali na bandari ya Dar es Salaam, mkoa wa Kigoma – uliopo kaskazini magharibi mwa Tanzania karibu na fukwe ya Mashariki ya ziwa Tanganyika – pia ni lango kuu la kibiashara kati ya Tanzania na DR. Congo.
Chanzo: BBC Swahili
Mipango na malengo ya Wizara ya Uvuvi.
Dira ya Sera ya Maendeleo ya Uvuvi ya mwaka 2015 inalenga kuwa na Sekta ya Uvuvi ambayo ifikapo mwaka 2025 itakuwa inachangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi na kuboresha maisha ya wananchi kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi.
Kilichofanyika kuboresha sekta ya Uvuvi kupitia Wizara ya Uvuvi.
Mradi wa SWIOFISH
Mradi wa kikanda uliotekelzwa katika nchi tatu za Tanzania, Msumbiji na Comoro katika awamu ya kwanza ya miaka 6 mradi huu ulianza kutekelezwa 22 Juni 2015, chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia kwa thamani ya US $ 36 milioni sawa na shilingi billion 97 865 499 240 za kitanzania na mradi umetekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Ilichofanya serikali.
Kufadhili njia za kisasa za ukaushaji wa Dagaa.
Katika kuboresha sekta ya uvuvi serikali kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) imejenga vichanja 80 vya kukaushia dagaa (Drying Racks), kununua mitambo minne (4) ya umeme ya kukaushia dagaa (Electric Drier) na Solar Tents 15 katika Halmashauri za Kilwa, Mafia, Pangani na Bagamoyo kuanzia mwaka wa fedha 2023/24.
Kuondoa viza kati ya Tanzania na Congo DR.
Mnamo mwezi Septemba,Serikali ya Tanzania ilitangaza kuondoa viza kwa raia wote wanaotoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo). Uamuzi huu unawafanya raia wa nchi hizo kuwa na uhuru zaidi wa kuingia na kutoka kwa ajili ya biashara na mambo mengine.
Mwanasiasa wa upinzani wa chama cha ACT Wazalendo na Mbunge wa zamani wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe aliandika kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter: “Kwa Miaka zaidi ya 10 nimekuwa nikipigania suala la wananchi wa Kongo (DRC) kuingia nchini Tanzania bila malipo ya viza na vile vile Watanzania kwenda DRC bila malipo ya viza. Hiki kilikuwa ni kilio kikubwa cha wafanyabiashara wa Kigoma ambao soko lao kubwa ni DRC. Nimefurahi sana kuwa hatimaye malipo ya viza yamefutwa. Biashara ya ukanda wa Ziwa Tanganyika itashamiri sana.”
Umuhimu wa dagaa kwa lishe na uchumi wa taifa unathibitishwa na uamuzi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO), kutoa waraka maalumu kuhusu Uvuvi Endelevu kwa lengo la kupunguza upotevu wa samaki na dagaa kwa kuhakikisha kitoweo hicho kinakuwa salama kwa soko zuri.