Mpango wa Ofisi ya Umwagiliaji Pangani.
19 October 2022, 2:50 pm
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekusudia kuanzisha Ofisi ya umwagiliaji wilayani Pangani ili kusaidia sekta ya kilimo wilayani humo ambayo imeonekana kuathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi huku wahanga wakubwa wakitajwa kuwa ni wakulima wadogo
Katika mahojiano maalumu aliyofanya na Pangani FM Afisa kilimo wa Halmashauri ya wilaya ya Pangani Bw. Ramadhani Zuberi amesema kuwa kupitia Mbunge wa Jimbo ambaye pia ni waziri wa maji Mh. Jumaa Aweso suala hilo limefika kwa Waziri wa kilimo ili kuifanya wilaya ya Pangani kuwa na Ofsi ya umwagiliaji na waziri huyo ameahidi kuleta wataalamu hivyo suala hilo lipo katika mchakato wa awali.
Hata hivyo Afisa huyo amesema kuwa tayari Halamshauri ya wilaya ya Pangani Umwagiliaji Pangani imepokea pembejeo za bure kwa ajili ya zao la Korosho hivyo mkulima anachotakiwa kufanya ni kusafisha shamba lake ili apatiwe pembejeo hizo na kupulizia ili kudhibiti magonjwa.
“Tumepata pia usaidizi kwenye mazao ya matunda haswa machungwa na maembe tulipata viwatilifu vya kuzuia wadudu na tayari tumegawa katika kata zinazozalisha matunda” – Ramadhani Zuberi Afisa Kilimo Pangani
Sekta ya kilimo ni tegemeo la kiuchumi kwa wananchi wa pangani ambao 80% ya wakazi wa wilaya hiyo ni wakulima na wafugaji wadogowadogo.