Pangani FM kuongeza nguvu katika Sensa 2022
20 June 2022, 7:09 pm
Kituo cha Redio Pangani FM kilichopo wilayani Pangani mkoani Tanga kinatarajia kuongeza nguvu katika kuisaidia serikali kufanikisha zoezi la sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Hayo yameelezwa na mhariri wa kituo hicho Bw. Erick Mallya kufuatia mafunzo maalum waliyopatiwa wahariri wa redio jamii zilizopo Tanzania nzima.
Mafunzo hayo yaliyolenga kuwaongezea uwezo wahariri wa Redio Jamii katika kufanikisha zoezi la Sensa ya watu na makazi 2022 yamefanyika katika Ukumbi wa MEDIA CENTER uliopo katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa Iringa tarehe 16-17 Juni,2022.
“Kwanza kabisa niwashukuru NBS na TADIO kwa kuwezesha mafunzo haya ya wahariri wa Redio Jamii kwa sababu hii inaenda kuongeza nguvu katika kazi ya Redio jamii kuripoti kuhusu Sensa lakini pia kuiwezesha jamii kufahamu kwanini tunafanya Sensa mwaka huu ikiwa wote tunafahamu kuwa Sensa ya mwaka huu n ya kipekee imekuja na mabadiliko mengi ikiwemo matumizi ya Tehama laini pia mwaka huu kwa mara ya kwanza itafanyika sensa ya majengo Tanzania kwa hiyo mabadiliko haya imekuwa vizuri kuwakutanisha wahariri wa Redio jamii ambao wanafanya kazi moja kwa moja na jamii ambayo wakati mwingine haifikiwi kirahisi na njia nyingine za mawasiliano na Habari hii inakwenda kuboresha Habari na Vipindi vya Sensa katika Redio Jamii”
Pichani Mhariri wa kituo cha Redio Pangani FM Bw. Erick Mallya pamoja na Mkufunzi wa Sensa ya watu na makazi ngazi ya Taifa 2022 Bi. Amina Ramadhani.
Kwa upande wake mmoja wa watoa mada kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi. Hellen Hilary amesema Sensa ya Watu na Makazi itasaidia Serikali kupanga mipango ya Maendeleo kwa kuzingatia takwimu zitakazokusanywa.
Baadhi ya mada zilizotolewa kwa Wahariri hao ili kuwajengea uwezo ni pamoja na; Sensa na Sheria ya Takwimu, Umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi na Maandalizi yake, Sensa na Mbinu za Uripoti kwenye Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 na Matumizi ya Mitandao ya Kijamii.
Sensa ya Watu na Makazi itafanyika Agosti 23, 2022 kote nchini ikilenga kusaidia kuongeza kasi ya maendeleo.
Sikiliza zaidi sauti hapo chini
.