Wanaume wa Pangani na malezi ya Watoto.
20 June 2022, 6:32 pm
Wanaume wilayani Pangani Mkoan Tanga wamepewa wito wa kutimiza vyema wajibu wao katika malezi ya watoto bila ubaguzi wa kijinsia.
Wito huo umetolewa na baadhi ya kina mama wilayani humo ambao kwa wamezungumza na Pangani FM.
Wanawake hao wamedai kuwa mara kwa mara wamekuwa wakitupiwa lawama kutokana na mienendo hasi ya watoto kwenye Jamii hususan mienendo ya watoto wa kike hivyo wamewataka wanaume kushiriki kikamilifu kwa kuweka msisitizo na kuwatazama watoto wa kike kama wanavyowatazama wakiume hivyo kuweka msisitizo katika malezi yatakayowafanya kuwa bora zaidi.
Pangani FM imezungumza pia na Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Pangani Magharibi na Mashariki Bi. Alfrida Kitandala ambaye amesema kuwa ni vyema wazazi kwa pamoja wakashirikiana katika malezi ya watoto bila kutupiana lawama.
“Jamii itambue kuwa malezi ni ya kwetu wote sio mtoto akiteleza na kukosea anyooshewe mama kidole na sio Mama na Baba tu Jamii nzima inahusika kwenye malezi ya mtoto unapoona mtoto amekosea wewe mwanajamii chukua hatua na umuelekeze yule mtoto kwa kushirikiana na wazazi wake sio muwe wa kwanza kunyoosha kidole kuwa Mama yake ndio anapelekea mtoto kuwa vibaya kufanya hivyo kunamuathiri Mwanamke na kumvunja Moyo Mwanamke” – Bi. Alfrida Kitandala