Pangani FM

Ubalozi wa Ireland wafanya ziara Pangani.

24 May 2022, 8:08 pm

Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania jana umefika hapa wilayani Pangani Mkoani Tanga ili kujionea Shughuli mbalimbali zinazofanywa na Shirika la UZIKWASA ambalo linafadhiliwa na mpango maalum wa Serikali ya Ireland wa misaada ya maendeleo ya kimataifa [Irish Aid].

 

 

 

 

 

 

Akizungumzia ugeni huo mkurugenzi wa Shirika la UZIKWASA Bwana Novatus Urassa amesema kuwa ujio huo ni sehemu ya maandalizi ya ziara ya Katibu Mkuu wa IRELAND anayetarajiwa kuitemmbelea Wilaya ya Pangani mapema mwezi ujao ili kujionea shughuli zinazofanywa na shirika hilo.

 

Balozi Mary O, Neil amepokelewa pia na viongozi wa wilaya ya Pangani wakiongozwa na mkuu wa wilaya hiyo Bwana Ghaibu Buller Lingo ambao waliambatana naye katika ziara hiyo.

 

Nao baadhi ya  wanufaika wa shirika la UZIKWASA wakizungumza mbele ya Balozi huyo katika Kijiji cha Kimang’a wameushukuru ubalozi wa Ireland  pamoja na shirika la UZIKWASA kwa namna wanavyochangia katika kutengeneza kizazi bora kwa ustawi wa jamii ya Pangani pamoja na kuwezesha mapambano dhidi ua ukatili wa wanawake na watoto.

Baadhi ya wanufaika hao ni waendesha pikipiki maarufu kama Bodaboda, Kamati za MTAKUWWA, wawezeshaji ngazi ya Jamii, viongozi wa ngazi mbalimbali za Serikali, walimu, wanafunzi na wasanii wa sanaa za maigizo.

Naye Balozi wa Ireland hapa nchini Bi. Mary O, Neil ameelezea kufurahishwa kwake kwa namna makundi mbalimbali yanayopatiwa mafunzo na shirika la UZIKWASA yalivyoweza kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta mabadiliko katika vijiji vyao.

Pia balozi Mary O. Neil amepongeza jitihada hizo na kusisitiza juu ya kuzifanya kuwa endelevu.

Katika hatua nyingine Balozi huyo ametembelea mradi wa unenepeshaji wa samaki aina ya kaa wa kikundi cha Jifute unaowezeshwa na shirika la IUCN ambalo pia linafadhiliwa na IRISH AID.

Balozi Mary O. Neil ametembelea pia Hospitali ya wilaya ya Pangani ambayo ia imekuwa mnufaika wa IRISH AID.