Historia mpya.
19 March 2021, 11:42 am
Leo, Machi 19, 2021 saa nne asubuhi aliyekuwa Makamu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma, Ikulu mkoani Dar es Salaam kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Historia Mpya: Rais wa kwanza Mwanamke Tanzania
Mama Samia alikuwa Makamu wa Rais wa kwanza Mwanamke Tanzania na wa pili kwa Afrika Mashariki.
Anakuwa Rais wa tatu mwanamke Afrika waliopitia mchakato wa kidemokrasia na wa kwanza kwa Afrika Mashariki.
Mwaka 2015, Rais Dkt John Pombe Magufuli alimchagua Samia Suluhu Hassan kuwa Mgombea Mwenza katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 na baada ya uchaguzi huo aliapishwa kushika Wadhifa wa Makamu wa Rais.
Historia hiyo ikajirudia tena Oktoba mwaka 2020 baada ya wawili hao kushinda uchaguzi Mkuu na kushika nafasi hiyo kwa muhula wa pili.
Samia Suluhu Hassan amekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha Dkt John Magufuli Machi 17 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu cha 37 (5), endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kutokana na maradhi ya mwili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano.
Kisha baada ya kushauriana na chama cha siasa anachotoka, Rais atapendekeza jina la mtu atakayekuwa Makamu wa Rais na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura zisizopungua asilimia hamsini ya Wabunge wote.