TANESCO yaomba radhi kukatika kwa Umeme Pangani.
11 March 2021, 9:24 am
Shirika la Umeme Tanzania Wilayani Pangani Mkoani Tanga limewaomba radhi wateja wake kipindi hiki Matengenezo ya Miundombinu yakiendelea kwenye maeneo mbalimbali Wilayani humo.
Akizungumza na PANGANI FM Meneja wa TANESCO Wilayani Pangani Bwana Saidi Shabani Muhando amesema kuanzia Mwezi February wamekuwa wakiendelea kukarabati Miundombinu ya umeme kufuatia muda mrefu kupita tangu Marekebisho kama hayo yalipofanyika.
Tangu mwezi wa February hadi mwezi huu tulionao tulikuwa tunaendelea na ukarabati wa line zetu kwa ajili ya maboresho ya umeme, kwanini tunafanya hivi? Tunafanya hivi kwa sababu mara ya mwisho kufanywa ukarabati kama huu ilikuwa ni mwaka 1996.
Sasa tumepata fursa hiyo, tumeona tufanye ukarabati huu katika maeneo yote ya wilaya, kwa hiyo niwaombe radhi sana wananchi na kuwapa pole katika kipindi hiki cha mpito tukiendelea na ukarabati.
Amesema Bwana Saidi
Hata hivyo Bwana Saidi amesema kukatika kwa umeme mara kwa mara sio tatizo la Pangani pekee, bali lipo pia kwenye maeneo mengine Nchini kutokana na Ukarabati unaofanyika katika mitambo yetu ya kufua umeme ya ubungo na songes wanakarabati yale mabomba ya kupitishia gesi.
Aidha Meneja huyo amewataka wananchi wanaoandaa mashamba kuwa makini pindi wanapochoma majani, kwa kuangalia Miundombinu ya umeme iliyopita kwenye Mashamba yao.
Hivi sasa tunapata changamoto ya kukatika umeme kwa sababu pia wananchi wanachoma moto na kuunguza nguzo na kusababisha usumbufu mkubwa wa kukatika umeme kwa muda mrefu, mfano Jumaamosi iliyopita kule kirare ilitokea hiyo, pale Ushongo wananchi wamefanya hivyo pia kule Madanga Juzi hivyo hivyo, sasa tunawaasa wananchi wanaoandaa mashamba kuwa makini na Miundombinu yetu iliyopita kwenye Mashamba yao.
Amesema Bwana Said
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Pangani Bi. Zainab Abdallah Issa amewataka wananchi wa Pangani kuwa na subira kwani suala la kukata kwa umeme mara kwa mara sio tatizo la Pangani pekee na linatokana na Matengenezo makubwa yanayofanyika Kitaifa.
Suala la kukatika kwa umeme ni nchi nzima, mimi juzi nilikuwa kwenye kikao cha wadau wa elimu wa mkoa kikao kilifanyika kule lushoto yaani ilikuwa kila dakika moja umeme unakata unarudi, hata pangani tuna nafuu kule lushoto hali mbaya, hapa nchini kila sehemu wanalalamika.
Amesema Bi ainab Abdallah
aidha Mkuu wa Wilaya ya Panganii ameongeza kuwa changamoto hiyo kubwa na ni suala ambalo liko nje ya uwezo wa TANESCO
Kwa hiyo tumegundua kumbe changamoto kubwa ni haya matengenezo makubwa ambayo yanafanyika kitaifa suala ambalo huyu meneja hapa lipo nje ya uwezo wake,Kwahiyo changamoto kubwa iliyojitokeza ni kwamba sasa hivi Tanesco wanafanya matengenezo Nchi nzima kwa wakati mmoja, lakini tayari Waziri mwenye dhamana ameshatoa maagizo kwamba anataka ndani ya wiki moja hili suala liwe limekwisha, kwahiyo wananchi wangu tuendelee kuwa na subra kwa sababu umeme mnapoona unakata kwenu hata kwangu unafanya hivyo hivyo.
Amesisitiza Bi Zainab Abdallah