Pangani FM

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ireland kutembelea Pangani.

3 June 2022, 12:02 pm

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ireland, Bw. Joe Hackett, anafanya  ziara nchini Tanzania kuanzia tarehe 3 mpaka 5 Juni 2022, akiambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Ireland (Irish Aid), Bw. Michael Gaffey. Ziara hiyo imekuwa ni fursa muhimu kwa Katibu Mkuu kushiriki na kushuhudia shughuli za Ubalozi, ushirikiano, na miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Ireland nchini Tanzania. Ziara hii imekuja kipindi ambacho Ubalozi wa Ireland unajiandaa kuzindua Mkakati wake wa mwaka 2022–2026, ambao unaendeleza mahusiano ya Ireland na Tanzania yaliodumu kwa miaka 43. Mkakati huo unategemewa kuchangia kiasi cha Euro 110 milioni kwa kipindi cha miaka mitano ijayo kupitia Ubalozi wake jijini Dar es Salaam.

 

 

Siku ya Ijumaa, tarehe 3 Juni 2022, Katibu Mkuu amefanya mazungumzo na Mhe. Liberata Mulamula, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, akiambatana na Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Bi. Mary O’Neill. Baada ya mazungumzo hayo, ujumbe wa Katibu Mkuu umefanya ziara ya siku mbili katika mikoa ya Pwani na Tanga, kutembelea miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Ireland.

Wilayani Bagamoyo (Mkoa wa Pwani), Katibu Mkuu amekutana na Mhe. Zainab Abdallah Issa, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo; Bw. Shauri Selenda, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo; na Bi. Kasilda Jeremiah, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo. Pia, ujumbe huo wa Katibu Mkuu ulitembelea makazi ya Bi. Halima Dumba, mnufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) ambao Ireland inachangia fedha. Pia, ujumbe huo ulikutana na maafisa ambao wanatekeleza mpango huo.

Wilayani Pangani (Mkoa wa Tanga), ujumbe wa Katibu Mkuu Joe Hackett umetembelea kijiji cha Kimang’a ambapo walishuhudia shughuli za wanajamii na shirika la UZIKWASA ambalo linatekeleza mradi wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake na wasichana. Baada ya hapo, Katibu Mkuu ametembelea Hospitali ya Wilaya ya Pangani ambayo Ireland inafadhili kupitia Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health Basket Fund). Ujumbe huo pia umetembelea mradi mpya wa uchumi wa buluu ambao unasaidia katika utunzaji wa mazingira na kipato endelevu cha wanajamii unaotekelezwa na Shirika la IUCN mkoani Tanga na Kisiwa cha Pemba (Zanzibar). Katibu Mkuu alikutana na kikundi cha kijamii cha vijana, kinachoitwa JIFUTE, na kujifunza kuhusu unenepeshaji wa kaa na kusikia mpango wao wa kutanua wigo wa shughuli zao.