Ziara ya Waziri Mkuu Tanga: Wakulima wa Mkonge washauriwa kuanzisha Ushirika.
20 January 2021, 3:36 pm
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha zao la mkonge linaendelezwa na kuwanufaisha watu wote wanaoshughulika na zao hilo.
Waziri Mkuu amesema hayo akiwa ziarani Mkoani Tanga wakati wa mkutano ulioshirikisha Wadau mbalimbali wa zao la mkonge, Mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Regal Naivera uliopo Tanga Mjini.
Amesema kwa sasa uhamasishaji unaendelea ili watu wengi zaidi wajishughulishe na kilimo cha mkonge na kwa kufuata ushauri wa Wataalam wa kilimo.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, Serikali inaendelea kufanya jitihada kubwa kuhakikisha zao la Mkonge linalimwa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Waziri Mkuu pia amewashauri Wakulima wa zao la mkonge katika maeneo mbalimbali nchini kuunda ushirika, ambao utawasaidia katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata mikopo itakayowawezesha kukuza kilimo hicho.