Mama Valerie: Uzoefu wa miaka 20 Pangani, namna ya kuheshimu tamaduni za wengine
21 May 2023, 1:02 pm
Ni muhimu sana kuvaa nguo vizuri kulingana na mazingira yako, mimi navaa tofauti sana nikiwa Uingereza kuliko hapa, Tanzania hasa Pangani kuna waumini wengi wa dini ya Kiislamu, sio vizuri kuvaa kaptura ni muhimu sana kuwa na heshima kwa tamaduni na desturi za wengine, ikiwa mtu ana mtoto mimi naona ni vizuri kumfundisha kuwa sisi sote ni binadamu, kila sehemu kuna tamaduni tofauti awe na heshima kwa kila mtu.
Amesema Bi. Valerie McGivern.
Na Erick Mallya
Tarehe 21 Mei kila mwaka, ni siku ya kimataifa ya anuwai za kitamaduni kwa mazungumzo na maendeleo, dhumuni la siku hii iliyowekwa na Umoja wa Mataifa ni kuangazia sio tu utajiri wa tamaduni za ulimwengu, lakini pia jukumu muhimu la mazungumzo ya kitamaduni kwa ajili ya kufikia amani na maendeleo endelevu.
Lakini kwani huu utofauti wa tamaduni ni nini hasa? Na una umuhimu gani? Je watu hujifunza vipi kuzoea tamaduni za wengine?
Kuyafahamu yote hayo nimezungumza na Bi. Valerie McGivern, yeye ni mzaliwa wa jiji la Manchester, nchini Uingereza, alikuja Pangani takribani miaka 20 iliyopita, mpaka sasa amelowea hapa Pangani, amejifunza mengi na amefundisha mengi kwa watu wa Pangani, anafahamika na watu wengi ndani na nje ya wilaya ya Pangani kutokana na kuendesha shule ya awali na msingi Children of Choba iliyopo katika kijiji cha Choba wilayani Pangani mkoani Tanga, ambayo imezalisha watu wenye taaluma mbalimbali kama ualimu, sheria, afya, n.k.
Picha: Mhariri wa Pangani FM Bw. Erick Mallya akizungumza na Bi.Valerie McGivern
Sikiliza hapa mazungumzo hayo
Sauti ya Mazungumzo kati ya Mwandishi wa Habari Erick Mallya na Bi. Valerie McGivern.
Picha: Bi. Valerie McGivern akiwa na moja ya wanafunzi wahitimu wa shule ya Choba katika mahafali ya Chuo cha Sheria IJA Lushoto.