Jinsi msimu wa uvuvi unavyosaidia kupunguza matukio ya wizi Pangani
13 December 2023, 11:26 am
Katika msimu wa uvuvi naweza kupata hata shilingi laki tatu kwa siku kwa kuuza dagaa, pia changamoto ya vijana kuiba yamepungua.
Na Cosmas Clement.
Kuanza kwa msimu wa uvuvi wa dagaa katika mji wa Pangani kumetajwa kuwa ni fursa nzuri kwa wakazi wa mji huo katika kuwawezesha kujipatia kipato cha siku.
Msimu huo wa uvuvi unaoanza mwezi wa tisa mpaka mwezi wa nne huwawezesha wavuvi kuendesha shughuli za uvuvi wa samaki aina mbalimbali ikiwemo dagaa uono katika bahari ya hindi mjini Pangani kwa urahisi tofauti na miezi mingine.
Wakizungumza na Pangani FM baadhi ya wanajamii wilayani Pangani wamesema tangu kuanza kwa msimu huo wa uvuvi wamekuwa wakiingiza kipato kizuri cha siku na kusaidia familia zao.
Pamoja na kuongeza kipato, wakazi hao wamesema msimu wa uvuvi umesaidia kupunguza changamoto za wizi kwa kuwa vijana wanapata chanzo cha mapato.
Shughuli ya uvuvi ni miongoni mwa shughuli muhimu kwa kuingiza Uchumi wa watu wa pangani pamoja na kuwa chanzo muhimu cha kuingizia mapato halmashauri ya wilaya ya Pangani.