Mimba za utotoni zaendelea kumkwamisha mtoto wa kike
11 October 2023, 4:49 pm
Picha kwa hisani ya mitandao ya kijamii
“Watoto wetu wamekuwa wakibakwa, wamekuwa wakipata mimba za utotoni hili ni eneo ambalo tunataka kusimamia kwa miguu miwili kupaza sauti kwa kushirikiana na wadau wengine ili elimu iwafikie watu wengi na hivi vitendo vikomeshwe”
Na Hamis Makungu
Changamoto mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni zimeendelea kuwa kikwazo kwa mtoto wa kike wilayani Pangani mkoani Tanga.
Hayo yamesemwa na Afisa Ustawi wa Jamii Pangani Enock Kirigiti wakati dunia ikiadhimisha siku ya mtoto wa kike iliyobeba kauli mbiu isemayo “Wekeza katika Haki za Mtoto wa Kike: Uongozi wetu, Ustawi wetu”.
Amesema changamoto kama ubakaji, ndoa na mimba za utotoni zimeendelea kukatiza ndoto na maendeleo ya mtoto wa kike wilayani Pangani.
Amesema atahakikisha kupitia sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009, mtoto analindwa dhidi ya changamoto zinazomkabili ikiwemo za ukatili na kupata haki zake za msingi.
Awali akizungumza na Pangani FM kuhusu siku ya mtoto wa kike, mmoja wa watoto wa kike wilayani Pangani Pili Salehe, amezitaja changamoto ambazo bado zinamkabili mtoto wa kike wilayani humo.
Siku ya “Mtoto wa Kike” huadhimishwa kila mwaka October 11 ambapo kwa mwaka huu kitaifa imefanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam na mgeni rasmi akiwa Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson.