UZIKWASA yaadhimisha Kipekee Siku ya Wanawake Duniani 2023
9 March 2023, 8:38 pm
Katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya wanawake 2023 yenye kauli mbiu isemayo ‘Ubunifu na mabadiliko ya teknolojia, chachu katika kuleta usawa wa kijinsia’. Shirika la UZIKWASA kwa mara ya kwanza limetoa nafasi kwa kamati za mazingira kuonyesha kwa umma mipango kazi yao inayohusisha masuala ya kijinsia na mbinu wanazotumia kutunza mazingira.
Na Erick Mallya
Shirika la UZIKWASA lililopo wilayani Pangani Mkoani Tanga jana katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Dunani Machi 8, 2023 limewakutanisha wadau mbalimbali wa masuala ya Jinsia, Mazingira, na Mabadiliko ya Tabianchi katika Tamasha kabambe lililofanyika katika kijiji cha Stahabu kilichopo wilayani Pangani.
Wanufaika mbalimbali wa afua za Shirika hilo wameshiriki na kupata nafasi ya kuonyesha mbele ya umma mafanikio yao, uzoefu na mbinu wanazotumia katika kupmbana na ukatili wa wanawake na watoto pamoja na utunzaji wa mazingira.
Wanufaika hao ni wajumbe wa kamati za mpango kazi wa taifa wa Kutokomeza tkatili dhidi ya wanawake na watoto za vijiji 33 vya wilaya ya Pangani, wawezeshaji ngazi ya Jamii na Wajumbe wa kamati za mazingira.
Vikundi vya Sanaa vikiongozwa na kikundi maarufu cha Sanaa za jukwaani cha ‘Banja Bas’ pamoja na kundi la muziki wa kizazi kipya la wachunguzi walipata nafasi ya kufanya maonyesho mbalimbali yaliyobeba ujumbe dhdi ya ukatili wa kijinsia na mabadiliko ya tabianchi.
Wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya wilaya ya Pangani, Mkoani Tanga na nje ya nchi wameshiriki katika tamasha hilo.
Kwa mara ya kwanza katika maadhimisho hayo Shirika la UZIKWASA limeikutanisha kamati ya mazingira ya kijiji hicho mara baada ya kuijengea uwezo katika kuhusisha masuala ya kijinsia katika mipango kazi yao.