RUWASA Maswa yatakiwa kusajili pikipiki kwa namba za serikali
8 May 2024, 4:16 pm
Vyombo vya watoa huduma wa maji ngazi ya jamii wilayani Maswa vimesaidia upatikanaji wa maji vijijini kutoka asilimia 68.9 hadi 74 na ifikapo 2025 kufikia asilimia 85.
Na, Daniel Manyanga
Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyoge amemtaka meneja wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini RUWASA wilayani hapo kuhakikisha pikipiki zilizokabidhiwa kwa watoa huduma wa maji ngazi ya jamii zinasajiliwa kwa namba za serikali ili ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa.
Aswege Kaminyoge ametoa rai hiyo wakati akizungumza na baadhi ya watoa huduma wa maji ngazi ya jamii waliokabidhiwa pikipiki hizo nne aina ya TVS 150 zenye thamani ya zaidi ya milioni kumi na sita ili kusaidia upatikanaji wa huduma ya maji hasa kwa jamii ya vijijini wanayoihudumia na siyo kufanya kazi isiyokusudiwa na serikali.
Kaminyoge amemtaka meneja wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini RUWASA wilayani hapo kufanya utafiti wa maji katika kata ambazo hazina maji ya uhakika ili kuweza kuwanusuru wananchi na adha ya upatikanaji wa maji wakiwa wanasubiri mradi mkubwa wa ziwa Victoria ambapo kuna bajeti ya milioni mia moja kwa ajili ya utafiti wa maji katika kata ambazo zinachangamoto ya maji.
Kwa upande wake afisa maendeleo ya jamii wa RUWASA wilayani hapo, Wilson Magaigwa amesema kuwa RUWASA imefanikiwa kuunda vyombo vya watoa huduma za maji ngazi ya jamii 7 kwa mjibu wa sheria namba 5 ya mwaka 2019 hivyo kuongeza upatikanaji wa maji vijijini hadi asilimia 74 kutoka 68.9 ya hapo awali.