Pangani FM

Zaidi ya Milioni 65 zimetolewa kwa wanawake,vijana na wenye ulemavu Pangani.

5 January 2021, 3:22 pm

Halmashauri ya Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii imefanikiwa kutoa Mikopo ya zaidi ya Shilingi Milioni 65 kwa Wanawake, Vijana na Walemavu katika kipindi cha nusu ya Mwaka wa fedha 2020/21.

Akizungumza katika mahojiano maalum na kituo hiki leo Bi. Mariam Ally kutoka Idara hiyo akiambatana na Afisa Maendeleo ya Jamii (W) Bwana Elias Msuya amesema kuwa kiasi hicho cha fedha kimetolewa kama Mkopo kwa makundi hayo kupitia asilimia 10 za mapato ya ndani ya Halmashauri.

Afisa Maendeleo Jamii Halmashauri (W)Pangani Bw. Elias Msuya pamoja na mradtibu wa Dawati la Jinsia (W) Bi.Mariam Ally katika Studio za Pangani FM Januari 5 2021

“Sisi kama Idara ya Maendeleo ya Jamii tumepokea maombi ya mikopo na tumeweza kutoa 65,368,000 kwa makundi ya vijana , wanawake na walemavu katika kundi la wanawake ni vikundi 10.vijana vikundi 3 na walemavu vikundi 3, kwenye kutoa tunatoa kwa mtindo wa 4-4-2 kwamba vijana 4%, wanawake 4% na walemavu 2%. Kwa wanawake tumetoa 29,450,000, Vijana 28,750,000 na walemavu 7,168,000.”

Amesema Bi. Mariam

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Wilayani humo Bw. Elias Msuya amesema kuwa mafanikio yaliyopelekea utoaji wa mikopo hiyo yametokana na usimamiaji mzuri wa makusanyo ya fedha za ndani.