Sibuka FM
Sibuka FM
11 March 2026, 2:21 pm

“Hatuwezi kupoteza fedha za walipa kodi kwa watu wasiokuwa waaminifu wanaokuja kwa kuomba mikopo kwenye halmashauri zetu wanapewa ikifika wakati wa marejesho wanaingia mitini lazima tuwe na sheria kali katika kulinda kodi za wananchi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.”
Na,Daniel Manyanga
Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Dkt.Vicent Naano Anney amevitaka vyombo vya sheria kuwafikisha mahakamani wale wote walipata mikopo ya asilimia kumi ya mapato ya ndani ya halmashauri na kushindwa kurejesha kwa wakati ili kuwapatia fursa vikundi vingine kupata mikopo hiyo.

Dkt.Annery amesema kuwa kuna vikundi vilipata mikopo hiyo kwa lengo la kujiinua kiuchumi kutokana na shughuli wanazozifanya lakini mpaka sasa hivi havijarudisha mikopo hiyo kwa ajili ya kuwapatia wengine mikopo huku zaidi milioni mia saba ikiwa mikononi mwa watu wasiokuwa waaminifu katika kurejesha mikopo isiyokuwa na riba.
Mkuu huyo ameongeza kuwa haiwezekani watu wachache wakope kwa lengo la kujiinua kiuchumi halafu ikifika wakati wa kurudisha wanatokomea kwingine bila kurejesha hivyo hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa vikundi ambavyo havijarejesha mikopo ikiwemo kuwaburuza mahakamani kama sheria inavyosema.

