Sibuka FM
Sibuka FM
24 February 2026, 11:38 am

“Tunahitaji kuwa na umeme wa uhakika ili kuvutia wawekezaji wakubwa kwenye viwanda maana hatuwezi kuwa na wawekezaji wakubwa wakati huo hatuna umeme wetu wa uhakika lazima sasa juhudi zifanyike kwa namna yoyote ile”.
Na,Daniel Manyanga
Wakazi wa mkoa wa Simiyu wameiomba serikali kupitia shirika la umeme Tanzania TANESCO kukamilisha ujenzi wa kituo cha kupozea umeme ili waweze kupata huduma hiyo kwa uhakika tofauti na sasa ambapo kumekuwepo na changamoto ya kukatikakatika hali inayopelekea baadhi ya vitu vyao vya ndani kuungua.
Wakizungumza na Sibuka Fm,Ali Sharifu,Amos Omolo na Wiliam Kiwango wamesema wanategemea umeme kufanya shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato lakini wapo ambao ni wateja wa bidhaa zinazotegemea umeme hivyo kukatika kwa umeme mara kwa mara kumekuwa changamoto kubwa kwao kufanya shughuli hizo.
Anamringi Macha ni mkuu wa mkoa wa Simiyu amesema kuwa wawekezaji hususan wa viwanda wanataka umeme wa uhakika ili wafaye uwekezaji utakaowapatia tija hatua itakayowezesha kuchangia kwenye pato la Taifa kutokana na uzalishaji huo.

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa TANESCO,Lazaro Twange amesema mkataba wa awali ulisainiwa 2023 kutoka na changamoto mkataba wake ulivunjwa na sasa utekelezwaji wake unafanywa na wataalamu wa ndani kutoka shirika la umeme Tanzani (TANESCO) kwa gharama ya shilingi bilioni 7 na walianza utekelezaji Oktoba 30,2025 na unatarajia kukamilika Mei 23,2026 na kwasasa umefikia asilimia 20.75.
Mkurugenzi mtendaji wa shirika la umeme Tanzania Lazaro Twange akiwa Malampaka wilayani Maswa kwenye eneo la ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa kilomita 110 inayotoka Ibadakuli mkoani Shinyanga hadi Imalilo wilayani Bariadi mkoani hapa kilipo kituo cha kupozea umeme ,na ujenzi huo ulianza March 2023 na unatarajiwa kukamilika Juni 30 2026 na utekelezaji wake umefikia asilimia 54.9.