Sibuka FM

RC Macha akabidhi mtambo wa kisasa jeshi la zimamoto na uokoaji

19 February 2026, 1:03 pm

Kwenye picha aliyevaa shati jeupe na madoa meusi ni mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha akikata utepe tayari kukabidhi mtambo huo wa kisasa kwa jeshi la zimamoto na uokoaji wilaya ya Maswa Picha kutoka maktaba ya Sibuka Fm

Kuna wilaya zingine hazina hata gari la zimamoto la kisasa kama hili lenye uwezo mkubwa wa kubeba tani tano lakini sisi tumepata lazima sasa hapo tukatunze sana huo mtambo ili uwasaidie wananchi pale ambapo panapotokea changamoto ya moto tuweze kuzima ili kuzuia madhara kwa wananchi.”

Na,Daniel Manyanga 

Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Anamringi Macha amelitaka jeshi la zimamoto na uokoaji mkoaa hapo kulitunza gari jipya la zimamoto lililokabidhiwa kwa jeshi la zimamoto na uokoaji wilayani Maswa ili liweze kufanya kazi iliyokusudiwa na serikali hususani majanga ya moto yanapotokea katika kuzima ikiwa ni mtambo wa kwanza tangu uwepo wa wilaya hiyo kongwe yenye zaidi ya miaka 100 ambapo mtambo huo umegharimu shilingi bilioni 1.3.

Pichani ni muonekano wa nje wa mtambo huo wa kisasa wa zimamoto na uokoaji uliokabidhiwa kwa jeshi la zimamoto na uokoaji wilaya ya Maswa ili kuweza kusaidia kukabiliana na majanga ya moto kama ikitokea Picha kutoka maktaba ya Sibuka Fm

Anamringi Macha ametoa maagizo hayo wakati wa kukabidhi mtambo huo kwa jeshi la zimamoto na uokoaji wilaya ya Maswa na kuongeza kuwa ni vyema mtambo huo ukatunzwa ili kuweza kuwahudumia wananchi katika kukabiliana na majanga ya moto pamoja na kuhakikisha kwa mamlaka zinazohusika na miundombinu ya barabara hasa vijijini zinakarabati miundombinu hiyo ili kuwezesha gari hilo liweze kupita bila shida yoyote.

Sauti ya mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha

Wakizungumza na kipindi hichi baada ya makabidhiano hayo baadhi ya wananchi walioshuhudia hafla hiyo,Suzana Shindah,Benard Mgindi na Yunisi Sayuni wamesema kabla ya ujio wa mtambo huo walikuwa wakitumia mbinu za kiasili ikiwa ni pamoja na kutumia mchanga, kupiga yowe ili kukusanya watu kusaidia kuzima moto hivyo kuishia kupata hasara ya kuunguliwa na vitu vyote kutokana na mbinu duni za kuzimia moto.

Sauti ya wananchi wakielezea natarajio yao baada kupokea mtambo huo wa kisasa wa zimamoto
Pichani ni kaimu kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Simiyu mrakibu msaidizi wa jeshi hilo, Faustin Mtitu akizungumza jambo na waandishi wa habari baada ya kupokea mtambo huo Picha kutoka maktaba ya Sibuka Fm

Kwa upande wake kaimu kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Simiyu, ASF Faustin Mtitu na mbunge wa jimbo la Maswa mashariki, Dkt.George Lugomela wamesema kuwa mtambo utasaidia sana katika kuzima moto pale ambapo ikitokea kutokana na mtambo huo kuwa na uzito mkubwa kwa ujazo wa maji pekee kg 5,000 sawa na tani tano hivyo uhitaji wa barabara za uhakika ikiwa ni sambamba na kuhitaji maji ya uhakika.

Sauti ya kaimu kamanda wa zimamoto na uokoaji mkoa wa Simiyu na mbunge wa jimbo la Maswa mashariki