Sibuka FM
Sibuka FM
13 February 2026, 12:52 pm

“Hatutakuwa na uvumilivu kwa watendaji wazembe ambao watakuwa sehemu ya kukwamisha ukusanyaji wa mapato ya halmashauri tunataka ufanisi zaidi katika kukusanya mapato ili kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi”.
Na,Daniel Manyanga
Baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu limepitisha mapendekezo ya bajeti ya zaidi ya shilingi bilioni 39 katika mwaka wa fedha 2026/27 kama matumizi ya utekelezaji wa shughuli za miradi ya maendeleo, matumizi ya kawaida na mishahara katika halmashauri hiyo.
Akizungumza na Sibuka Fm katika kikao cha baraza la madiwani mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Mayala Lucas amesema baraza limepitisha bajeti ya zaidi ya shilingi bilioni 39 katika mwaka wa fedha 2026/27 huku watumishi wakikumbushwa kusimamia ukusanyaji wa mapato ili kufikia malengo ya halmashauri iliyojiwekea.
Awali akizungumza katika kikao hicho kaimu mkuu wa idara ya mipango wa halmashauri hiyo, Sayi Luseba ametoa mchanganuo wa bajeti hiyo, huku kaimu mkurugenzi wa hamlashauri hiyo, Albert Siogopi amesema kuwa watahakikisha wanasimamia ukusanyaji wa mapato kwa ufanisi mkubwa.
Kwa upande wao baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo akiwemo,Deogratius Mayala, Emmanuel Maseko na Charles Lyaganda, wameeleza walivyojipanga kusimamia suala la ukusanyaji wa mapato ili kufikia malengo yaliyowekwa na halmashauri ya wilaya ya Bariadi.